Na.Arusha DC
Msimamo wa Serikali ya awamu ya sita katika kukuza sera yake ya Diplomasia ya Uchumi, imeendelea kuifungua nchi kwani taasisi ya SALMIN AFRIKA yenye makao makuu yake Dubai kwa kushirikiana na Taasisi ya KGB FUND- VIETNAM zimekuja Mkoani Arusha kwa lengo la kuangalia fursa za uwekezaji zitakazowashirikisha wazawa.
Akizungumza wakati wa kikao hicho cha uwekezaji, Rais wa Taasisi ya SALMIN AFRIKA Profesa Salmin Ibrahim Salmin amesema kuwa, kazi kubwa ya Taasisi yake ni ushauri wa kiuwekezaji pamoja na kuwatafuta wawekezaji wakubwa wenye mitaji pamoja na Taasisi za kifedha zenye riba nafuu ili kuwaunganisha na Watanzania ambao wana makampuni yaliyosajiliwa ili waweze kuingia makubaliano ya uwekezaji.
Profesa, Salmin ameeleza kuwa, Tanzania imebahatika kuwa na fursa nyingi za uwekezaji hivyo kwa kutambua hilo, wameona ni vyema kuwaunganisha Watanzania na fursa za mikopo ya riba nafuu pamoja na wawekezaji wakubwa wenyewe mitaji kwa lengo la kufanya uwekezaji na biashara kwa ushirikiano wa pamoja. “Kampuni ya KGB FUND ya Vietnam ni moja ya kampuni tuliyoileta nchini na iko tayari kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya kilimo cha mpunga, ufugaji na uvuvi wa samaki, uanzishaji wa viwanda vya samani zinazotokana na mbao, uchimbaji madini pamoja na ununuzi wake, ujenzi wa mahoteli pamoja na nyumba za makazi, biashara ya utalii pamoja na viwanda vya kusindika matunda na chakula”, ameweka wazi.
Kwa upande wa mikataba ya uwekezaji na biashara, Profesa Salmin amesema Taasisi yake itafuata Sheria na taratibu za nchi katika masuala ya uwekezaji kwa kuhakikisha kampuni za wazawa wanaotaka kuingia nao mikataba ya ushirikiano, zinakuwa na leseni halali za kibiashara pamoja na kutumia taratibu za kibenki katika kuwawezesha wale wote watakaofuzu vigezo vya kupata mikopo ya riba nafuu na yenye marejesho ya muda mrefu.
Akizungumzia fursa za uwekezaji zilizopo Mkoani Arusha hususan katika Halmashauri ya Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, ndugu Seleman Msumi amesema Halmashauri inayo maeneo yanayofaa katika uwekezaji wa mahoteli, nyumba za makazi, viwanja vya michezo, maeneo ya kujenga masoko ya kisasa, ujenzi wa vituo vikubwa vya magari ya abiria na mizigo, maeneo ya ujenzi wa vituo vya afya vya kutolea huduma ya dharura pamoja na kumbi za mikutano ya kimataifa. Maeneo hayo yapo burka A na B, Gomba Estate, Mateves, Ngaramtoni, Likamba pamoja na Mlangarini.
Msumi anasema, maeneo hayo yapo kwenye ukanda maalum kiuwekezaji na kuwa yametengwa mahususi ili kuongeza vitega uchumi vya Halmashauri, ambapo moja ya jukumu kubwa la Halmashauri hiyo ni kubuni vyanzo vipya vya mapato pamoja na kukusanya maduhuri kupitia vyanzo hivyo.
Aidha, ndugu Msumi pamoja na kuipongeza Taasisi hiyo kwa kuonyesha dhamira ya kuwaleta wawekezaji na kutafuta Taasisi za kifedha zenye riba nafuu, pia amewataka kuzingatia taratibu na Sheria za uwekezaji hususan wakati wa utengenezaji wa mikataba, ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima wakati wa utekelezaji wake.
Itakumbukwa kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mh.Dkt Samia Suhulu Hassan tangu kuingia kwake madarakani, imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali ikiwemo kufanya mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje, ili kuimarisha uchumi wetu kama nchi hasa baada ya kutoka katika janga la uviko 19.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.