Na Elinipa Lupembe
Serikali ya awamu ya sita, kupitia halmashauri ya Arusha imekabidhi viti mwendo vinne kwa wanafunzi wenye ulemavu kutoka shule nne zenye vitengo vya elimu maalum, viti ambavyo viwarahisishia wanafunzi hao shuguli zao binafsi na zili za kimasomo kwa uhuru na amani.
Akizungumza wakati akikabidhi viti mwendo hivyo, kwa walimu wakuu na wazazi wa watoto hao, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi amesema kuwa, msaada huo umepunguza changamoto ya watoto hao kutembea hasa wakiwa katika mazingira ya shule kutokana uwezo wao mdogo wa kutembea, jambo ambalo lilisababisha udhaifu katika kujifunza na kufundishika wawapo shuleni.
Aidha Mkurugenzi Msumi ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia wanafunzi wengine wenye uhitaji wa namna hiyo ili watoto hao waweze kutimiza ndoto zao.
“Tuna uhitaji mkubwa wa vifaa kwa ajili ya kuwahudumia hawa watoto wawapo shuleni, hivyo nitoe wito kwa yeyote atakayeguswa kutoa msaada akaribie katika ofisi zetu za halmashauri au katika mojawapo ya shule zenye watoto wenye uhitaji wa namna hiyo ili waweze kutoa msaada huo”. Alisisitiza Mkurugenzi Msumi.
Hata hivyo wazazi wa watoto hao waliopatiwa msaada, wameishukuru serikali kwa kuendelea kuwakumbuka wahitaji kwa kuwa sasa watoto hao wataendelea kupata elimu bila changamoto iliyokuwa inawakabili hapo awali ya kukaa pamoja na kusogea kutoka sehemu moja hadi nyingine.
“Ninamshuru Rais Samia Suluhu kwa kunipatia hiki kiti ambacho kitanisaidia kusoma bila changamoto, mama alinibeba kunipeleka shuleni, alikuwa anachoka sana, na wakati mwingine hakunipeleka, naamini nitatimiza ndoto yangu ya kuwa Mhasibu”. Amesema Catherine Paul, mtoto mwenye ulemavu wa darasa la 3 shule ya msingi Naurei
Kwa upande wao walimu wakuu wa shule hizo wameishukuru na kuipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwakumbuka na kuwajali watoto hususani wenye mahitaji maalum na kuahidi kushirikiana na wazazi wa watoto hao kuvitunza hivyo viti mwendo ili viweze kudumu na kuwasaidia wanafunzi hao kwa muda mrefu.
“Tunatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na serikali hasa kwa kutoa fedha ya chakula kila mwezi kwa watoto wenye ulemavu na sasa imeona umuhimu wa kuwaletea viti mwendo, licha ya kuwa uhitaji bado ni mkubwa lakini tumepata sehemu ya kuanzia”. Alisema Mwl. Getruda Tarimo, Mwalimu Mkuu shule ya Msingi Naurei.
Awali, halmashauri ya Arusha inakabiliwa na uhaba wa viti mwendo zaidi ya ishirini (20) katika shule nane zenye vitengo vya Elimu Maalum, pamoja na vifaa vingine kwa ajili ya kuwahudumia hao watoto.
ARUSHA DC
KaziInaendelea
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.