Na Elinipa Lupembe
Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imetoa jumla ya vitabu vya kiada kwa shule zote za sekondari halmashauri ya Arusha lengo likiwa kuendelea kuboresha miundombinu ya ufundishaji na ujifunzaji kwa walimu na wanafunzi shuleni.
Akizungumza wakati akikabidhi vitabu hivyo kwa wakuu wa shule za sekondari, mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Selemani Msumi amesema kuwa halmashauri imepokea jumla ya vitabu vya kiada 26,186 kwa ajili ya shule zote 35 za serikali huku shule tatu mpya za kata zikipokea vitabu 2,720 vya kwa mara ya kwanza na kufanya kwa uwiano wa 1:1 kila mwanafunzi kutumia kitabu chake.
Mkurugenzi Msumi licha ya kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwekeza fedha nyingi za kuboresha miundombinu ya shule za sekondari, amesema kuwa, uwepo wa vitabu shuleni utarahisisha tendo la kufundisha na kujifunza na kuwawezesha wa wanafunzi kujisomea na kupata maarifa zaidi hatimaye kufikia malengo yao ya kitaaluma.
Aidha ametoa wito kwa walimu na wanafunzi kuvithamini vitabu hivyo kwa kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa pamoja na kuvitunza ili viweze kutumiwa sasa sasa na vizazi vijavyo.
"Niwatake walimu kusimamia utunzaji na matumizi sahihi ya vitabu hivi na sio kuvifungia stoo, hakikisheni wanafunzi wanavitumia wakati wote wa masomo, huku kukiwa na utaratibu mzuri wa kuviazima na kuvirudisha mara baada ya kuvitumia" Ameagiza Msumi
Hata hivyo wakuu wa shule wameishukuru serikali kwa kuendelea kuimarisha sekta ya elimu kwa kuhakikisha kuna kuwa na majengo mazuri, vifaa vya kujifunzia pamoja na vitabu vya kiada kwa masomo yote tofauti na miaka ya nyuma changamoto zilikuwa ni nyingi lakini zinaendelea kumalizika siku hadi siku.
Mkuu wa shule ya sekondari Kiutu, Mwl. Upendo Mollel, amesema licha ya kuwa shule yao ni mpya lakini kwa kipindi kifupi serikali imewapa vitabu 1,158 ambapo kila mwanafunzi atatumia kitabu chake mwenyewe jambo ambalo litawaongezea ari ya kujifunza.
"Kabla ya kuwa na vitabu wanafunzi walisoma kwa shida, kitabu 1 wanafunzi 10, wakati mwingine walishindwa kufanya vizuri masomo yao kwa kukosa vitabu vya kufanyia 'reference' uwepo wa vitabu utawapa fursa wanafunzi kujisomea kwa nafasi na kupata maarifa hata baada ya kufundishwa na walimu darasani" Mwl. Jackson Mpinga, Mkuu wa shule sekondari Olomitu
Naye mkuu wa shule sekondari Olturoto, Mwl. Peter Mlinga, amekiri kuwepo tatizo la upotevu wa vitabu shuleni kutokana na uzembe na kuahidi kuandaa mpango mzuri wa utunzaji wa vitabu kwa kumkabidhi kitabu mwanafunzi kwa maandishi na kuhakikisha anatumia na kukirudisha kwa wakati.
Naye Afisa Elimu Taaluma Mwl. Editha Chona, amefafanua kuwa katika mgao huo, wa vitabu 26, 186, shule tatu za mpya za sekondari za kata zilizosajiliwa kati ya mwaka 2020 na 2023 zimepata vitabu 2,720 vya masomo yote, ikiwa ni pamoja ma shule shule ya sekondari Olturoto vitabu 873, sekondari Kiutu vitabu 1,158 na shule ya sekondari Olomitu vitabu 689.
Ikumbukwe kuwa huu ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala ya kuhakikisha mazingira bora ya shule za serikali nchini zikiwa na miundombinu bora, ikiwemo madarasa, maabara za masomo ya Sayansi na TEHAMA na vifaa vyake, maktaba pamoja na vitabu vya kiada na ziada..
ARUSHA DC NI YETU, TUHSIRIKIANE KUIJENGA
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.