Na. Elinipa Lupembe.
Shirika lisilo la kiserikali la Community Aid and Social Education Empowerment -CASEE, kwa ufadhili wa shirika la Child Fund Korea -CFK la nchini Korea, limekabidhi msaada wa vishikwambi 55, (tablet), kwa shule ya mchepuo wa kiingereza ya Enaboishu Academy, shule inayomilikiwa na halmshauri ya Arusha, lengo likiwa ni kuunga mkono juhudi za za serikali la kurahisisha na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa walimu na wanafunzi nchini.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Meneja Miradi, shirika la CASEE, Ombeni Sakafu amesema kuwa, wametoa msaada huo wa vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia kwa shule ya msingi Enaboishu Academy, vyenye thamani ya shilingi milioni 30.7, mara baada ya kupata taarifa, toka kwa mkurugenzi wa halmashauri ya Arusha, ya kuwataka wadau kujitokeza kuchangia, maendeleo ya shule hiyo mpya ya mchepuo wa kiingereza, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza na kupandisha taaluma katika shule hiyo na halmashauri kwa ujumla wake.
Sakafu amefafanua kuwa, shirika la CASEE, linafanya kazi kwa kushiriki mipango na malengo ya serikali iliyopo madarakani, kuboresha na kuweka mazingira rahisi na salama ya wanafunzi kujifunzia, hasa kwa kutumia teknolojia ya kisasa, ili kufikia lengo la serikali la kuhakikisha mtoto wa kitanzania anapata elimu bora katika mazingira bora.
"Licha ya kurahisisha tendo la kujifunza na kufundisha kwa kutumia teknolojia ya kisasa, lakini pia CASEE ina lengo pia kuhamasisha wanafunzi kupata masomo kwa njia ya mtandao 'e-learning' na TEHAMA kwa ujumla, tukiamini kujifunza kwa njia ya dijitali, vifaa hivi vitasaidia wanafunzi kupata ujuzi na maarifa, wakati mwingine bila kuwa na mwalimu" amesisitiza Sakafu
Naye Kaimu Mkurugenzi halmashauri ya Arusha na Afisa Elimu Msingi, Hossein Mghewa, amelishukuru shirika hilo la CASEE, kwa kutoa vifaa hivyo vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia, vifaa ambavyo vitarahisisha kazi ya kujifunza na kufindisha kwa walimu na wanafunzi, kwa kuwa vishikwambi hivyo vina programu yenye vitabu vya kiada na ziada, jambo ambalo litapunguza changamoto ya upungufu wa vitabu katika shule hiyo.
"Vishikwambi hivi, vina programu yenye vitabu vya kiada vyenye masomo yote, pamoja na vitabu vya ziada ambavyo vitawaongezea wanafunzi maarifa zaidi kwa urahisi zaidi na gharama nafuu, katika masomo". Amefafanua Kaimu Mkurugenzi huyo.
Hata hivyo Mwalimu mkuu wa shule hiyo ya Msingi Enaboishu Academy, Rajabu Mfutakamba, amesema kuwa, vifaa hivyo ni muhimu sana kwa wanafunzi katika tendo la kujifunza kwa kutumia teknolojia rahisi na ya kisasa, teknolojia ambayo itawezesha kuwajengea maarifa kupandisha kiwango cha taaluma shuleni hapo.
Mkuu huyo wa shule ameweka wazi kuwa, vishikwambi hivyo vina programu zenye vitabu vya kiada vya masomo yote, vitabu vya ziada kwajili ya kuongeza maarifa katika masomo yao, pamoja na programu maalumu kwa wanafunzi wa awali wanaoanza kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu, maarufu kama KK tatu.
"Tablet hizi zitasaidia kuwaongezea wanafunzi ari na kasi ya kujifunza pamoja na uwezo wa kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu kwa haraka na wepesi, kutokana na programu yenye kumpa mwanafunzi uwezo wa kusoma na kuandika maneno 200 kwa muda wa dakika 40" amefafanua Mwalimu Mfutakamba
Shirika la CASEE limetoa Vishikwambi 55, kwa shirika la CFK la nchini Korea kufadhili vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milion 30.7, huku fedha hizo zikijumuisha gharama za vishikwambi 55, vikiwa na kifurushi muhimu 'full package', pamoja na kiasi cha fedha hizo, kugharamia mafunzo na miongozo ya namna ya kutumia vishkwambi hivyo, kwa walimu wa shule hiyo, ambayo yanaendelea kufanyika.
PICHA ZA MAKABIDHIANO YA VIFAA HIVYO
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.