Na. Elinipa Lupembe.
Viongozi wa jamii, halmashauri ya Arusha, wamesema kuwa kuna haja ya kutoa elimu kwa jamii yao, juu ya masuala ya afya zao, ili kuweza kujikinga na maambukizi ya magonjwa pamoja na kuzuia madhara makubwa zaidi yanayoweza kutokea kwa jamii kutokana na ukosefu wa elimu ya afya.
Viongozi hao, wamesema hayo wakati wa kikao kazi cha utambulisho mradi wa TULONGE AFYA unaojihusha na masuala ya afya, unaotekelezwa na shirika lisilo la kiserikali la 'Empowerment of Marginalized Community' - EMAC, kwa ufadhili wa Idara ya Maendeleo ya nchini Marekani, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa SOS eneo la Ngaramtoni.
Akizungumza mara baada ya kuelezwa lengo la mradi, Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha, mheshimiwa Noah Lembris amesema kuwa, kuna haja kubwa kwa jamii kupata elimu zaidi juu ya afya zao, jambo ambalo litawawezesha wananchi kutambua namna ya kujikinga na magonjwa pamoja na kuepusha madhara yanayotokana na ufahamu mdogo juu ya afya zao.
Amesisitiza kuwa, endapo mradi wa TULONGE AFYA utafanyika vizuri, unaweza kusaidia kuimarisha afya za wananchi, bila kutumia gharama kubwa na kuahidi kutoa ushirikiano kwa shirika hilo ili wananchi waweze kupata elimu hiyo ya afya, itakayoleta mabadiliko chanya kwenye jamii yao.
Akizungumza wakati wa kutambulisha mradi huo, mratibu wa mradi, Gervas Mollel, amesema kuwa lengo la mradi wa TULONGE AFYA ni kuwajengea wananchi uwezo kuwa na tabia chanya za afya ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha kina mama wajawazito na wenzi wao kuhudhuria Kliniki mapema na kupata huduma na ushauri muhimu wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua na zaidi kuwahimiza kujifungulia katika vituo vya afya na sio kwa wakunga wa jadi.
Kuwahamasisha vijana miaka 15-24 juu ya afya ya uzazi na kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuingia kwenye mahusiano ya ngono au ya ndoa ikiwa na lengo la kujikinga na maambukizi ya magonjwa, mimba na ndoa za utotoni.
"Vijana wengi katika umri huu wapo kwenye hatari ya kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi, mimba za utotoni zisizo tarajiwa na athari nyingine juu ya afya zao, zinazofifisha na kuua ndoto zao na kupoteza dira ya maisha yao" amesema Mollel
Mollel amethibitisha kuwa TULONGE AFYA umejikita zaidi kwenye mambo manne ambayo ni pamoja na Afya ya Uzazi, maambukizi ya VVU na UKIMWI, ugonjwa Malaria na Kifua Kikuu.
Hata hivyo viongozi hao wa jamii, wamekiri ukosefu wa elimu ya kutosha kwa jamii juj ya Afya na kuongeza kuwa kuna umuhimu wa jamii yao kupata elimu hiyo kwa njia rahisi na isiyo rasmi.
Naye Afisa Afya wilaya Issa Msumari, amesema kuwa, mradi huo wa TULONGE AFYA, unategemea kutekelezwa kwa muda wa miezi saba, kwenye kata zote 27 za halmashauri ya Arusha kwa ushirikiano mkubwa wa watalamu wa ngazi ya wilaya, kata na vijiji na viongozo wa jamii wa ngazi zote za kata na vijiji na kuwafikia wananchi wote walengwa wa mradi huo ndani ya halmashauri hiyo.
Kikao kazi hicho, kimewakutanisha waheshimiwa madiwani wa kata zote 27, maafisa Watendaji wa kata zote, maafisa Afya wa kata zote na wataalamu wa afya ngazi ya halmashauri.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.