Na Elinipa Lupembe
Shirika la Kijiji kwa Kijiji la nchini Denmark, limekabidhi jengo la bwalo la chakula la kisasa, shule ya sekondari Oldonyowas, ujenzi uliogharimu shilingi milioni 157, lenye uwezo wa kuhudumia wanafunzi 200 kwa wakati mmoja.
Akikabidhi bwalo hilo, Mkurugenzi wa shirika la kijiji kwa kijiji, Jesper Gregersen, amesema anayo furaha kukamilisha ujenzi wa bwalo hilo, ambalo utaondoa adha ya muda mrefu waliyoipata wanafunzi ya kulia chakula nje, ambapo sasa wanafunzi watakula chakula kwa usalama kwenye eneo rasmi, zuri, safi na la kisasa.
"Leo ninafuraha kubwa kwa kuwa lengo tulilokusudia limetimia, Bwalo hili linauwezo wa kuchukua wanafunzi wengi kwa wakati mmoja na wakapata chakula bora na salama kutokana na uwepo wa miundombinu ya kisasa". Amesema Jesper
Ameongeza kuwa ujenzi wa jengo hilo umezingatia utunzaji wa mazingira kwa kuwa na jiko la kisasa linalotumia kuni chache lenye mfumo wa kuchemsha maji kwa kutumia nishati ya jua, hali inayochangia kupunguza kiasi cha kuni wakati wa kupika huku akisisitiza kuwa lengo la shirika hilo ni kushirikiana na serikali ya Tanzania kuwahudumia wananchi na watoto wa kitanzania ili wapate elimu bora kwenye mazingira rafiki.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa Bwalo hilo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Stedvant Kileo, licha ya kulishukuru shirika hilo kupitia mdau Jesper, ameweka wazi kuwa serikali inatambua na kuthamini michango ya wadau wa maendeleo katika sekta ya elimu, ambayo inawezesha kurahisisha upatikanaji wa huduma bora hususani kwa jamii zinazoishi vijijini.
Aidha ameutaka uongozi wa shule kuwasimamia na kuwaelimisha wanafunzi namna ya kuitunza miundombinu shuleni hapo, ili itumike kwa muda mrefu na idumu kwa vizazi hadi vizazi na kuwanufaisha watoto kutimiza malengo yao ya kielimu.
"Miundombinu ya shule hii ni mali yenu wananchi wa Oldonyowasi, serikali ni wasimamizi tuu, leo tumekabidhiwa bwalo likiwa linapendeza, lakini mnalo jukumu kubwa la kuendelea kushirikiana katika kuitunza ili miundombinu hii iendelee kuwanufaisha watoto wenu na vizazi vyenu vijavyo" Ameweka wazi Kileo.
Hata hivyo Mwenyekiti wa Kijiji cha Oldonyowas Mhe. Geofray Ayo, amemshukuru mfadhili wa mradi kupitia shirika la Kijiji kwa Kijiji, kwa kuwa amekuwa msaada mkubwa kwa shule hiyo kwa kufadhili miradi mingi inayowezesha mazingira rafiki kwa wanafunzi kuendelea kusoma kwa bidii na kukuza kiwango cha taaluma kwenye shuleni hapo.
Akionyesha furaha yake mpishi wa shule, Veronica Daudi ameeleza namna jiko hilo linavyomrahisishia shughuli zake za upishi tofauti na hapo awali alipokuwa akipika kwenye kibanda kidogo.
“Kwakweli nimefurahi sana, tangu nianze kutumia jiko hili nimekuwa na amani kwasababu jiko nililokuwa natumia awali lilikuwa ni kibanda kidogo, kilichojaa moshi, uliotishia afya yangu, kwa sasa niko kwenye jiko zuri ninafurahia kufanya kazi yangu". Amesema Veronica
Naye Mkuu wa Idara ya Elimu ya Sekondari, ameahidi kuendelea kusimamia vyema miundombinu hiyo sambamba na kusimamia maendeleo ya taaluma shuleni hapo ili wanafunzi waweze kufaulu vizuri na kufikia ndoto zao za kielemu.
Akisoma taarifa ya shule, mkuu wa shule ya sekondari Oldonyowas Mwl. Juma Bukwimba amesema kuwa, jengo hilo ni muhimu kwa wanafunzi, litarahisisha na kuokoa muda wa wanafunzi kupata chakula sehemu rasmi na salama lakini zaidi, litaongeza ari ya wanafunzi kusoma na ufaulu wa wanafunzi kuongezeka.
ARUSHA DC NI YETU, TUSHIRIKIANE KUIJENGA
Bwalo jipya
Jiko la zamani
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.