Shirika lisilo la kiserikali la SOS lenye makazi yake eneo la Ngaramtoni, linalojulikana kama Kijiji cha Kulea Watoto SOS, limekabidhi msaada wa vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 54 kwa ajili ya wananchi wa halmashauri ya Arusha, wilayani Arumeru.
Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo, Mratibu wa Miradi ya kuimarisha familia, Shirika la SOS, Innocent Estomihi, amesema kuwa, shirika lao, limejikita zaidi kuzijengea uwezo jamii zisizo na uwezo, katika ngazi ya familia ili zipate uwezo wa kujitegemea na kujipatia kipato, ambacho kiwawezesha familia hizo kujiinua kiuchumi.
Amefafanua kuwa, licha ya kuwa shirika hilo limejikita kuwahudhumia watoto yatima na wale walio kwenye hatari ya kupoteza familia, lakini pia shirika hilo, linahudumia familia zisizo na uwezo pamoja na kutoa misaada kwenye taasisi za serikali katika maeneo ambayo familia wanazozihudumia zinalazimika kupata huduma katika taasisi hizo.
Aidha ameitaja misaada iliyokabidhiwa imelenga kwenye sekta ya Elimu, Afya na Maendeleo ya Jamii, na kutaja misaada uliolenga sekta ya Elimu ni pamoja na Kompyuta 22 zenye thamani ya shilingi milioni 19 zilizotolewa kwenye shule ya Msingi Lemanyata na Engalaoni, huku wakikabidhi seti tatu za mashine za kukoboa na kusaga nafaka kwa vikundi vitatu vya wajasiriamali zenye thamani ya shilingi milioni 19.
Wamekabidhi pia vifaa tiba kwenye vituo 4 vya kutolea huduma za Afya, ikiwa ni pamoja na vitanda 7, vitanda 3 vya kujifungulia ' Delivery bed' na vitanda 4 vya kufanyia uchunguzi 'Examination bed', vifaa 4 vya kuchemshia gozi ' Sterlizer' pamoja na kifaa 1 cha kupimia ' Microscope', vyote vimegharimu kiasi cha shilingi milioni 16.
Hata hivyo Estomihi amesema kuwa, shirika lao haliko mbali na kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano, iliyojikita katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa hali ya chini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera licha ya kulishukuru shirika la SOS kwa misaada hiyo inayoipunguzia kazi serikali amewataka wananchi wote waliokabidhiwa misaada hiyo kuwa wazalendo na kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ili kupunguza na kuondoa kabisa changamoto zilizokuwa zinawakabili.
Amefafanua kuwa licha ya wahudumu wa Afya kukabiliwa na changamoto ya mazingira magumu ya kazi, amewasisitiza wahudumu hao kutumia vifaa hivyo, kuwahudumia wagonjwa na si vinginevyo na kuthibitisha kuwafuatilia kwa karibu na kuhakikisha, wahudumu hao watoa huduma bora kwa wagonjwa.
"Natambua mazingira magumu ya kazi, wekeni uzalendo mbele, tumieni vifaa hivi tulivyopewa kuwapatia wagonjwa huduma bora, tutaendelea kuwafuatilia na kuhakikisha kila mtalamu anatekeleza majukumu yake" amesema Dkt. Mahera
Awali Kijiji Kulelea Watoto - SOS Ngaramtoni kinajishughulisha na kuhudumia watoto waliopoteza wazazi na wale walio kwenye hatari ya kupoteza malezi, na kinahudumia familia 185 zinazoishi ndani ya kijijini na familia 15 zinazoishi nje ya kijiji kwenye familia zao.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.