Serikali ya awamu ya tano, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF awamu ya III, imeshusha neema ya kipekee kwa kutekeleza miradi mitatu kwa mpigo, kwenye kijiji cha Oldonyowas, kata ya Oldonyowas, halmashauri ya Arusha, wilayani Arumeru.
TASAF awamu ya III imeanza kutekeleza miradi hiyo mitatu, iliyojikita kwenye sekta ya elimu, kwa kujenga majengo mapya, katika shule mpya ya sekondari ya Oldonyowas, miradi yenye thamani ya shilingi milioni 229.5 shule ambayo inategemea kianza mapema mwaka ujao wa masomo wa 2019.
Akizungumza na mwandishi wetu ofisini kwake, Mratibu wa TASAF halmashauri ya Arusha, Grace Makema, amesema kuwa, tayari fedha za miradi hiyo, zimeingizwa na tayari mchakato na hatua za awali za ujenzi zimeanza, kwa ushirikiano wa kitengo cha TASAF, Idara ya ujenzi pamoja na kamati ya ujenzi ngazi ya kijiji.
Mratibu huyo amefafanua kuwa, miradi hiyo mitatu inajengwa kwenye shule mpya ya sekondari Oldonyowas na itahusisha ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa vitavyogharimu kiasi cha shilingi milioni 69.9, jengo la utawala milioni 92.1 pamoja na nyumba ya walimu yenye sehemu mbili kwa shilingi milioni 67.4.
Aidha mratibu huyo, ameongeza kuwa kufuatana na taratibubza utekelezaji wa miradi ya TASAF, mradi huo uliibuliwa na wananchi wenyewe wa kijiji cha Oldonyowas, kwa kuangalia zaidi kipaumbele chao, katika uhitaji wa kuwa na shule ya sekondari katika kata yao.
Hata hivyo mwenyekiti wa kijiji cha Oldonyowas mheshimiwa Geofray Akyoo, amethibitisha ushiriki wa wananchi katika uibuaji wa mradi huo, na kuishukuru TASAF kwa kuwaunga mkono, wananchi hao, kwa kuongeza nguvu za wananchi ambao tayari walikuwa wameanza ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa, ofisi ya walimu pamoja na choo cha matundu kumi na mbili.
Ameongeza kuwa lengo la kuanza ujenzi wa shule ya sekondari ambayo hapo awali haikuwepo katika kata yao, jambo ambalo limesababisha adha kubwa kwa watoto wao, kutembea umbali wa Kilomita 16 kwenda na kurudi shuleni na kuongeza kuwa, umbali huo umekuwa ukisababisha baadhi ya watoto kukata tamaa na kuacha shule.
" Lengo la kuweka kipaumbele cha kuwekeza kwenye mradi wa ujenzi wa shule, ni kutaka watoto wetu wasome hapa karibu na zaidi sisi wazazi tupate nafasi ya kufuatilia maendeleo ya watoto kwa karibu, watoto wetu wanateseka sana, wanatembea Kilomita 16 kwenda na kurudi kufuata elimu ya sekondari, watoto wengine wanakata tamaa na kuacha shule" amesema Mwenyekiti huyo
Hata hivyo Mwenyekiti Akyoo, ameongeza kuwa, tayari wameanza taratibu za usajili wa shule hiyo kwa kushirikiana na Idara ya Elimu sekondari na wanategemea shule hiyo, kuanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa mwaka wa masomo 2019.
Naye Msimamizi wa mradi kutoka Idara ya Ujenzi, halmashauri ya Arushs, Fundi Sanifu, Richard Mwatujobe, amethibitisha kuwa, ujenzi wa miundombinu hiyo uko hatua za awali na kasi ya ujenzi wa miundombinu yote, unaendelea vizuri na unategemea kukamilika mapema, mwishoni mwa mwezi Disemba mwaka 2018 na ifikapo Januari 2019, miundombinu hiyo kuweza kutumika.
Awali wananchi wa kijiji cha Oldonyowas walianza ujenzi wa shule hiyo mpya ya sekondari kwa gharama ya shilingi milioni 46 ambapo asilimia 30 ya gharama hizo ilikuwa ni nguvu za wananchi wa Oldonyowas huku asilimia 70, ziligharamiwa na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa TANAPA.
PICHA ZA HATUA ZA AWALI ZA UJENZI WA MAJENGO HAYO.
Hatua za awali za ujenzi wa majengo shule ya sekondari Oldonyowas
Mafundi wakiendelea na kazi ya ujenzi wa miundombinu ya shule ya sekondari Oldonyowas
Mafundi wakiendelea na ujenzi wa msingi wa jengo mojawapo la shule ya sekondari Oldonyowas.
Msingi wa jengo la vyumba vya madarasa
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.