Na Elinipa Lupembe
Kufuatia mkakati wa serikali ya awamu ya sita wa kutokomeza vifo vya wanawake na watoto wakati wa kujifungua kwa kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati na kila kata inakuwa na kituo cha afya, umefanyika kwa vitendo kwenye kata ya Bwawani halmashauri ya Arusha, kwa serikali kutoa shilingi milioni 357 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya Bwawani, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo kata ya Bwawani, Mkuu wa wilaya ya Arumeru Mhe. Emmanuela Kaganda Mtaifikolo, amethibitisha serikali kutimiza lengo la kutokomeza vifo vya kina mama na watoto wakati wa kujifungua kwa vijiji vyote vinne vya kata hiyo kuwa na zahanati huku sasa ikiendelea na ujenzi wa kituo kipya cha Afya Bwawani.
Amesema kuwa kutokana na Jiografia ya kata ya Bwawani, uwepo wa vituo vya kutolea huduma za afya ndani ya maeneo yao ni muhimu sana kwa kuwa licha ya kuwarahisishia upatikanaji wa huduma muhimu za afya, itaondoa vifo visivyo vya lazima hususani kwa kina mama na watoto wakati wa kujifungua na wananchi wote kupata huduma za afya katika maeneo yao.
"Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushusha fedha nyingi za utekelezaji wa miradi kwenye kata hii ya Bwawani, wananchi watanufaika na miradi hii, kutokana na ukweli kuwa walipata adha kubwa ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya, jambo ambalo kwa sasa litakuwa historia kwao" Amesema Mkuu huyo wa wilaya.
Hata hivyo wananchi wa kata ya Bwawani wamemshukuru pia Mhe. Rais kwa kuwajali na kuona umuhimu wa kuwapa fedha za kujenga kituo cha afya, mradi ambao haujawahi kutokea tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika.
Farida Msuya mkazi wa kijii cha Bwawani, ameweka wazi kuwa, kukamilika kwa kutuo hicho kutawaondolea adha wananchi hasa wanawake wajawazito, wanapopata changamoto wakati wa kujifungua na kulazimika kufuata huduma za afya Kituo cha afya cha Nduruma au mjini Arusha.
"Tunamshukuru mama Samia, tunamuombea kwa Mungu kwa kutuonea huruma na kutujengea kituo cha afya, kipindi cha nyuma wapo kinamama wenzetu walipoteza watoto na wengine maisha kwa kujifungulia nyumbani na wengine kuchelewa kupata huduma kutokana na umbali, kwa sasa tunaamini hakuna mama atajifungulia nyumbani na hakutakuwa na vifo visivyokuwa vya lazima" Amesema Esta Supatoi
JONAS Laiza, ameelezea matumaini makubwa ya kituo hicho kuwa, kitawasaidia wananchi kupata huduma ambazo hazikupatikani kwenye zahanati, kuna watoto wanaozaliwa kabla ya siku, huwa kwenye hatari kubwa ya kupoteza maisha wanapozaliwa kwenye zahanati, uwepo wa kituo cha afya utaokoa maisha ya watoto hao.
Awali Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Arusha, Selemani Msumi, amefafanua kuwa mradi huo unatekelezwa kwa shilingi milioni 357 ukijumuisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) milioni 143.7, milioni 121.2 wodi ya wazazi, na milioni 92.1 ujenzi wa nyumba ya watumishi yenye uwezo wa kuishi familia tatu (3 in 1), ujenzi uko kwenye hatua ya kupaua na unategemea kukamilika mwishoni mwa mwezi Oktoba 2023.
ARUSHA DC ni Yetu, Tushirikiane Kuijenga"
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.