Na. Elinipa Lupembe.
Katika kuboresha miundo mbinu ya kufundishia na kujifunzia kwenye shule za sekondari za kata, serikali kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania - TEA, imekamilisha ujenzi wa vyumba 3 vya madarasa, viti na meza 150, shule ya sekondari Sokon II, halmashauri ya Arusha wilaya ya Arumeru.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi shuleni hapo, mkuu wa shule sekondari Sokon II, mwalimu Prisca Mbele, ameweka wazi kuwa, kukamilika kwa vyumba hivyo vya madarasa, kumeondoa msongamano wa wanafunzi darasani na kuwezesha shule hiyo, kufikia malengo ya wastani wa wanafunzi 50, kukaa ndani ya chumba kimoja cha darasa, jambo ambalo limefanikisha mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia shuleni hapo.
Aidha Mkuu huyo wa shule amesema kuwa, ujenzi wa vyumba hivyo 3 vya madarasa umegharama kiasi cha shilingi milioni 60 kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania na kuongeza kuwa, licha ya kuondoa upungufu wa vyumba vya madarasa zaidi umeondoa msongamano wa wanafunzi madarani, na umewezesha shule hiyo kufikia mpango wa uwiano wa wanafunzi 50 kwa darasa moja.
"Tunaishukuru serikali kwa kuweka nguvu kubwa kuboresha miundombinu ya shule yetu, shule haina umri mkubwa tangu ianzishwe mwaka 2015, lakini ina miundombinu inayojitosheleza, tuna madarasa ya kutosha, shule ina vyumba 27 vya madarasa , maabara 3 za masomo ya Sayansi, maabara ya somo la ICT, ofisi za walimu, tuna jumla ya wanafunzi 978 wanaotumia vyumba 20 vya madarasa" amefafanua Mkuu huyo wa shule.
Naye mwalimu wa Taaluma shuleni hapo, mwalimu Geofrey John amesema kuwa, utoshelevu wa vyumba vya madarasa shuleni hapo, unawezesha walimu kuwafikia wanafunzi wote wakati wa kufundisha, jambo ambalo wanaamini litaimarisha kiwango cha taluma na kupandisha ufaulu shuleni hapo.
Hata hivyo mwalimu huyo wa taaluma, ameweka wazi, kuendelea kuimarika kwa ufaulu shuleni hapo, katika mitihani ya Taifa na kufikia 97.4 % kwa matokeo ya kidato cha nne, na 99.4% kwa matokeo ya kidato cha pili kwa mwaka 2021.
Denning Innocent mwanafunzi wa kidato cha pili, amethibitisha wanafunzi wote kufurahishwa na uwepo wa madarasa ya kutosha shuleni kwao, na kuthibitisha kuwa kunawapa nafasi ya kujifunza katika mazingira mazuri, na pia kunawaongezea ari ya kujifunza.
"Tunaishukuru serikali kwa kutujengea majengo mazuri shuleni kwetu, kwa sasa tunasoma kwenye mazingira mazuri,mhatuna tofauti na shule za 'private', kila mwanafunzi anakaa kwenye meza na kiti chake, nafasi ni kubwa darasani, tuna maabara za masomo yote ya Sayansi, tuna chumba cha ICT, hii inatupa moyo wa kusoma kwa bidii na kufaulu mitihani yetu ya Taifa" amesisitiza mwanafunzi Denning
Awali shule ya sekondari Sokon II, kata ya Kiutu ni miongoni mwa shule za kata inayokuwa kwa kasi kubwa, iliyoanzishwa kwa nguvu za wananchi mwaka 2015 huku Serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu ikiweka nguvu kubwa za kuhakikisha shule hiyo inakua kwa kasi na kutimiza ndogo za wazazi walioanzisha shule hiyo.
ARUSHA DC
#KaziInaendelea✍✍✍
#elimubilamalipo
#mamlakayaelimutanzania
Wanafunzi wa kidato cha pili shule ya sekondari Sokon II wakiwa darasani .
Hali ya chumba cha darqsa
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.