Na. Elinipa Lupembe.
Ubalozi wa Japani nchini Tanzania, umetoa kiasi cha dola za kimarekani 87,974 ikiwa ni takribani shilingi milioni 195 za kitanzanis, kwa ajili ya ujenzi wa jengo la ghorofa lenye vyumba vinne vya madarasa na samani zake, kwenye shule ya sekondari Sokon II halmashauri ya Arusha, wilayani Arumeru.
Hata hivyo, tayari Murugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera amesaini mkataba na balozi wa Japani nchini Tanzania Balozi, Shinishi Goto, katika hafla fupi iliyofanyika nyumbani kwa balozi huyo mapema wiki iliyopita.
Akizungumza wakati hafla hiyo, Balozi wa Japani, amesema kuwa, serikali ya Japani inashirikiana vema na serikali ya Tanzania, na inaona umuhimu wa kuunga mkono sera ya serilikali ya Tanzania ya kutoa elimu bila malipo kuanzia darasa la kwanza mpaka kidato cha nne, sera inayotekelezwa kwa kasi na kwa vitendo na serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Naye Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, amefafanua kuwa, kiasi hicho cha fedha, kilichotolewa na ubalozi wa Japani, kitawezesha ujenzi wa msingi wa ghorofa moja yenye vyumba 12 vya madarasaa, na kuwezesha kukamilisha msingi wa jengo hilo la ghorofa moja na kukamilisha vyumba vinne vya madarasa pamoja na samani za madarasa hayo kati ya vyumba 12 vya jengo zima.
Mkurugenzi Mahera, ameongeza kuwa, ukamilishaji wa miundombinu vyumba 12 vya madarasa vya shule hiyo, unahitaji kiasi cha shilingi milioni 330.2, ambapo kiasi cha shilingi milioni 90 kitatolewa na serikali kupitia wizara ya Elimu na shilingi milioni 50 zitatolewa na halmashauri kupitia mapato yake ya ndani.
" Ili kukamilisha jengo lenye vyumba 12 vya madarasa, tunahitaji shilingi milioni 330.2, hiyo serikali itashirikiana na ubalozi wa Japani kukamilisha ujenzi wa mradi huo" amesema Dkt. Mahera.
Mkuu wa shule ya sekondari Sokon II, mwalimu Mwamvita Kilonzo, amethibitisha uwepo wa changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa shuleni hapo, usiowiana na idadi kubwa ya wanafunzi waliosajiliwa shuleni hapi.
Amefafanua kuwa shule hiyo ina jumla ya wanafunzi 1,006, ikiwa na vyumba 11 vya madarasa, kukiwa na uhitaji wa vyumba vingine 11 ili kufikia vyumba 22 ambavyo vitawiana na idadi ya wanafunzi.
Mhandisi wa Ujenzi, halmashauri ya Arusha, mhandisi Bibie Manzi, amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo, uko katika hatua za awali ambapo mchakato wa kumpata mkandarasi umeshapatikana, na ujenzi unategemea kuanza mapema mwezi ujao wa Aprili na unategemea kukamilika mwishonj mwa mwaka huu wa 2019.
Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera (kushoto) na Balozi wa Japani nchini Tanzania Balozi Shinishi Goto (kulia) wakinyoosha juu mkataba wa milioni 195, mara baada ya kusaini kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa shule ya sekondari Sokon II.
Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera, wakisaini mkataba na Balozi wa Japani nchini Tanzania, Balozi Shinishi Goto, nyumbanj kwa Balozi huyo.
Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson Mahera, akizungumza wakati wa utiaji saini mkataba na Balozi wa Japani nchini Tanzania, nyumbani kwa Balozi huyo.
Picha ya pamoja ya wajumbe waliohudhuria utiaji wa saini ya mkataba na Balozi wa Japani nchini Tanzania, Balozi Shinishi Goto, nyumbani kwa Balozi huyo.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.