Na. Eliniap Lupembe.
Wadau wa maendeleo wa shirika la ABERCROMBIE & KENT PHILANTROPY (A&K) linalofanya shughuli zake mkoani Arusha, limetambua adha wanayopata wanafunzi wenye ulemavu, wanaosoma kwenye kitengo cha elimu maalum shule ya msingi Ilboru, halmashauri ya Arusha, kwa kukosa sehemu ya kulia chakula na kuamua kuwaondolea adha hiyo na kuwajengea Bwalo la chakula.
Wadau hao marafiki wa shule hiyo, licha ya kutoa misaada mingi katika kitengo hicho, wameanza ujenzi wa Bwalo la Chakula walilolipa jina la 'Dinning & Kitchen Project', mradi ambao unategemea kugharimu kiasi cha shilingi milioni 54 mpaka kukamilika kwake, mapema mwishoni mwa mwaka huu.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Ilboru mwalimu Ronald Mwende, amesema kuwa msaada huo wa ujenzi wa Bwalo la chakula, umekuja wakati wa muafaka kutokana na changamoto inayowajabili wanafunzi hao, ya kukosa mahali rasmi pa kulia chakula huku kituo hicho kina jumla ya wanafunzi 106 ambao wote wanapata chakula cha mchana shuleni, wakati wengine 65 wako bweni wakipata huduma ya chakula kwa muda wote.
"Ninawashukuru sana wafadhili wa A& K, kwa kuona umuhimu wa kujenga Bwalo, uwepo wa Bwalo utawafanya watoto hawa kupata chakula eneo ambalo ni rasmi na salama kiafya na kiakili pia, kwa kuwa watoto wenye mahitaji maalumu wanahitaji ungalizi wa hali ya juu muda wote tofauti na watoto wengine, hapa shuleni". Amefafanua mwali Mwende.
Hata hivyo, Diwani wa kata ya Ilboru Mhe. Lembris Ngiremo, amesema kuwa, Bwalo hilo litaeleta mapinduzi katika kata hiyo licha ya kutumika kwa ajili ya kulia chakula wanafunzi wenye mahitaji maalumu, lakini pia litatumika kama ukumbi zinapotekea warsha mbalimbali, kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa kata hiyo.
Aidha Diwani huyo, amewataka wadau mbalimbali kujitokeza kuungana na serikali kuendeleza miundombinu ya kitengo hicho cha Elimu maalumu, kutoka mwitikio mkubwa wa jamii na kupeleka watoto wao wenye ulemavu shule, jambo ambalo limesababisha ngezeko la watoto hao kuandikishwa shule, kutokana na serikali kuwapa fursa watoto wenye ulemavu kupata elimu kwa maendeleo ya taifa la Tanzania.
Naye Anastazia Pastori, mwanafunzi wa darasa la nne, mwenye ulemavu wa kusikia kwa mbali, amelishukuru shirika la A &K, kwa kujenga Bwalo la chakula na kusema kwamba, bwalo hilo ni muhimu sana kwao, kwa kuwa hawana sehemu maalumu ya kulia chakula.
Awali Anastazia, ameipongeza serikali kwa kuwajali watoto wenye ulemavu kwa kuwapa kiapaumbele kwenye masuala ya elimu na kuonheza kuwa yeye amefanikiwa kujua kusoma na kuandika kawaida pamoja na matumizi ya lugha ya Alama, lugha ambayo licha ya kumsaidia kimasomo inamuwezesha pia kuwasaidia watu wenye usonji.
"Nilianza kusoma Kitengo Maalum kwenye darasa la ufundi, baada ya kumudu stadi tatu za kuandika, kusoma na kuhesabu, nimeweza kujiunga na mfumo wa elimu ya kawaida na sasa niko darasa la nne, ninajiandaa na mtihani wa Taifa wa darasa la nne, nikiwa na wenzangu wasio na mahitaji maalumu, na ninahakika nitafanya vizuri" amesistiza Anastazia.Katika shule ya msingi Ilboru,
Kitengo hicho cha Elimu Maalumu, kilianza rasmi mwaka 2001 kikiwa na wanafunzi 6, mpaka sasa kitengo kina jumla ya wanafunzi 106, kikiwa na wanafunzi viziwi, usonji, ulemavu wa akili, ulemavu wa viungo na ulemavu wa ngozi (albinisim), huku wanafunzi 65 kati ya hao, wakiwa wanalala bweni 65, wavulana 45 na wasichana 40.
BWALO LA CHAKULA SHULE MSINGI ILBORU KITENGO MAALUM
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.