Wadau kutoka sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na mashirika ya dini, wanaojishughulisha na masuala ya afya ndani ya halmashauri ya Arusha, wameweka mkakati wa kushirikiana na halmashauri hiyo, kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya afya kwa sasa.
Wadau hao wameweka mikakati hiyo, wakati wa kikao kazi cha mwaka cha 'Private Partinership Performance (PPP)', kikao kilichojumuisha wadau wa afya na watalamu wa halmashauri ya Arusha, kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano halmashauri ya Arusha.
Wadau hao, wameazimia kwa pamoja kufanya matembezi shirikishi yatakayojumuisha wadau mbalimbali na wananchi wa maeneo husika, ambayo yatafanyika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, ikiwemo zahanati na vituo vya afya kwa lengo la kutafuta fedha za kuatua changamoto zinazo ikabili sekta hiyo ya afya.
Aidha wadau hao wameweka kipaumbele cha matembezi hayo, kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vilivyo kwenye , maeneo ya pembezoni mwa halmashauri hiyo, kwa kuwa huko ndiko kwenye changamoto kubwa, kulinganisha na maeneo ya mijini.
Akizungumza wakati wa kufungua kikao kazi hicho, kwa niaba ya mkurugenzi Mtendaji, Afisa Rasilimali Watu, halmashauri ya Arusha Mohamed Mavura, amewataka wadau wote wa afya ndani ya halmashauri hiyo, kushiriki kikamilifu kuisaidia serikali kutatua changamoto zinazoikabili sekata ya afya, ili kuhakikisha wananchi wote, wanapata huduma muhimu za afya katika maeneo yao kuanzia kwenye zahanati ndani ya vijiji vyao.
Mavura ameongeza kuwa sekta ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo kimsingi kuna baadhi ya changamoto ambazo, serikali inahitaji wadau kushiriki bega kwa bega kuzitatua.
Aidha amewataka wadau hao kushiriki katika, upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kutolea huduma za afya pamoja na ujenzi wa miundo mbinu ya vituo vya afya, kwa kuwa mpaka sasa halmashauri ina upungufu wa zahanati 20 kutoka zahanati 47 zilizopo ili kukamilisha uwepo za zahanati katika vijiji vyote 67.
"Serikali imeandaa mazingira rafiki ya ushiriki wa wadau katika kutatua changamoto za huduma za afya, hivyo niwatake wadau, mwisho wa kikao kazi hiki, tuweke mikakati ya pamoja ya namna ya kuinua sekta ya afya ndani ya halmashauri yetu, kwa kuweka vipaumbele katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wa maeneo ya pembezoni mwa mji" amesema Mavura.
Aidha Afisa Utumishi huyo, amethibitisha kuridhishwa na kazi kubwa inayoifanywa na wadau hao wa afya na kuwaomba kutochoka bali kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha ili waweze kuisaidia halmashauri na serikali kwa ujumla kutimiza malengo katika kuboresha sekta ya afya.
Naye Mganga Mkuu wa halmashauri ya Arusha Dkt.Petro Mboya amesema kuwa, licha ya changamoto zinazoikabili sekta ya afya, sekta hiyo imepata mafanikio makubwa kwa mwaka ulioisha, mafanikio yaliyotekelezwa na serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya, ikiwa ni pamoja na ongezeko la bajeti ya dawa kutoka shilingi milioni 764.9 mwaka uliopita wa 2017/2018 na kufikia shilingi milioni 861.2 kwa mwaka huu mpya wa fedha unaoendelea wa 2018/2019.
Aidha Dkt. Mboya ameongeza kuwa kwa, upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya umeimarika hadi kufikia asilimia 97, kuboreka kwa utoaji huduma za afya pamoja na kupunguza idadi ya vifo kwa mama na mtoto wakati wa kujifungua.
Hata hivyo wadau waote walioshiriki kikao kazi hicho, wameupongeza uongozi wa halmashauri ya Arusha kwa ushirikiano mkubwa unaotolewa kwa wadau hao na kuahidi kuendelea kushiriki kwa hali na mali kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya afya, huku wakisisitiza kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli.
Mdau kutoka shirika la Engender Health, Sebastian Macrice, amethibitisha ushiriki wa shirika lao, katika kutatua changamoto kama zilivyowasilishwa na Idara ya afya, huku akiwataka watalamu wa afya kujitoa kwa moyo kuwahudumia wagonjwa licha ya changamoto zilizopo.
................._________...........
PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA KIKAO KAZI
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.