Na. Elinipa Lupembe.
Wananchi na wafugaji wa kata ya Musa, halmashauri ya Arusha, wamejitokeza kwa wingi kuogesha mifigo yao, wakati wa hafla ya uzinduzi wa zoezi la kitaifa la kuogesha mifugo, uliofanyika kwenye josho la Oloitushula na kuahidi kuanza tabia ya kuogesha mifugo yao, mara baada ya Serikali kuwapatia dawa za kuogeshea mifugo na kutoa bei elekezi ya kuosha mifugo, ikiwa ni shilingi 50 kwa ng'ombe na shilingi 10 kwa mbuzi, kwa muosho mmoja, bei ambayo kila mfugaji anaweza kumudu.
Wananchi hao, wametoa ahadi hiyo, walipofika kuogesha ng'ombe wao kwenye Josho hilo, lililosimama kufanya kazi kwa muda, na kufunguliwa upya, ikiwa ni kampeni ya serikali ya awamu ya tano kuanza kuhamasisha upya, wafugaji kuogesha mifugo yao.
Wamesema, wamekuwa wakitumia gharama kubwa kununua dawa za kuogesha ng'ombe na mifugo mingine, pamoja na kutumia muda mrefu kuogesha ng'ombe, jambo ambalo lilikuwa likiwakatisha tamaa sana, na kudababisha baadhi ya wafugaji na kuacha kabisa kuogesha mifugo yao.
Mwenyekiti ya Kamati ya Josho la Olotushula, Malaki Meoki, amesema uwepo wa josho hilo, utawahamasisha wafugaji wengi kuogesha mifugo yao, kwani awali wengi walijikuta wakiacha kuogesha, kutokana na kushindwa kumudu gharama kubwa za kununua dawa hizo, jambo ambalo liliwasababishia wafugaji hasara ya mifugo yao kufa kutokana na magonjwa yaenezwayo na kupe na mbung'o.
"Kwa sasa Serikali imeturahisishia, bei ya shilingi mia na shilingi hamsini ni ndogo, kila mfugaji anaweza kumudu, tutasimamia na kuhakikisha ng'ombe wote wanaogeshwa ili kuwakinga na magonjwa yaenezwayo na kupe" amesema Mwenyekiti huyo.
Naye mfugaji Jonas Ivan, ameisema ujio wa dawa hizo ni neema kwao, kwani awali walilazimika kuogesha mifugo kwa kutumia bomba na kunyunyuzia dawa, jambo ambalo lilikuwa ni hatari kwa afya zao, hivyo wengi wao kushindwa kuosha mifugo, na kuahidi kwa sasa wataosha kwa kutumia josho ili kuepusha mifugo yao kufa na magonjwa yanayozuilika.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Halmashauri ya Arusha, wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo, Mkuu wa Idara ya mifugo, Charles Ngilorit, amewasisitiza wafugaji hao, kujenga tabia ya kuogesha mifugo ili kuzuia magonjwa yaenezwayo na kupe ,magonjwa ambayo huua mifugo kwa asilimia 75 kwa mwaka na kuwapa wafugaji hasara kubwa, huku taifa likipoteza pato la takribani shilingi milioni 63 kwa mwaka.
Amesema, Serikali ya awamu ya tano, imeanzisha upya kampeni hiyo kwa kutoa dawa bure kama mtaji kwa wafugaji, na kuzipa mamlaka Tawala za Mikoa na serikali za Mitaa, kuhamasisha wafugaji kuogesha mifugo pamoja na kusimamia uendeshaji wa majosho kupitia kamati za majosho na serikali za vijiji.
Amewashauri wajumbe wa kamati ya Josho kusimamia mapato na matumizi ya fedha zinazotokana na kuogesha mifugo, na kuwahimiza fedha zinazopatikana ziwekwe benki, nakutolewa taarifa zake, kwenye serikali ya kijiji na hatimaye kwa wananchi kupitia, mkutano mkuu wa kijiji.
Serikali imetoa dawa, na zoezi hili linatakiwa kuwa endekevu, halmashauri imepokea lita 75 za dawa na kugawa lita 10 kwa kila Josho, na kuwataka wafugaji kutumia fursa hiyo, kuokoa gharama kubwa za kununu gharama dukani na kuwathibitishia kuwa, licha ya kuwa kuogesha kwenye josho ni gharama nafuu, lakini pia, ni njia salama zaidi kiafya, kuliko ile ya kupulizia.
Aidha ameitaka serikali ya kijiji, kuwasimamia wafugaji kuogesha mifugo na kutambua kua, kuogesha mifugo ni suala la kisheria na ni lazima na sio hiari, hivyo wahakikishe wanawabana wale wote, watakaokiuka sheria hiyo.
"Tukiacha wafugaji wengine waogeshe na wengine wasiogeshe, bado tutakua na vimelea vya maambukizi ya magonjwa katika maeneo yetu, hivyo tushirikiane kwa pamoja kupambana na magonjwa hayo kwa kuhamasishana sisi kwa sisi kuogesha mifugo yetu na kuwabana watakao kiuka sheria" amesema Ngilorit.
Naye Kaimu Afisa Mtendaji wa kata ya Musa, Asheli Kiseli, amesema kuwa, kwa siku ya kwanza, mwitikio wa wafugaji kuogesha mifugo umekuwa mkubwa, na kufafanua kuwa, katika uzinduzi wa josho hilo la Oloitushula, jumla ya ng'ombe 1, 015, mbuzi 100 na kondoo 50 wameogeshwa.
*PICHA ZA MATUKIO WAKATI WA UZINDUZI*
Mkuu wa Idara ya Mifugo, Charles Ngilorit akipima dawa ya kuogeshea mifugo, tayari kwa kuichanganya kwenye josho, wakati wa uzinduzi wa josho la Oloitushula kata ya Musa.
...................................................................................
Mkuu wa Idara ya Mifugo Charles Ngilorit, akimimina dawa kwenye josho la Oloitushula kama ishara ya kuzinduzi upya josho la Oloitushula kata ya Musa.
...............................................................................
Baadhi ya ng'ombe wakiogelea kwenye josho la Oloitushula mara baada ya josho hilo kuzinduliwa upya.
................................................................................
Ng'ombe ambao tayari wamekwishaogeshwa, wakati wa uzinduzi wa josho la Oloitushula kata ya Musa.
...........................................................................................
Baadhi ya ng'ombe walioletwa kuogeshwa, wakati wa uzinduzi wa josho la Oloitushula kata ya Musa.
........................................................................................
Wafugaji wa kata ya Musa wakiwa na makundi ya ng'ombe zao, wakisubiri kuogeshwa, wakati wa uzinduzi wa josho la Oloitushula.
...................................................................................................
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.