Na Elinipa Lupembe
Wajumbe wa Kamati ya fedha Utawala na Mipango, halmashauri ya Arusha, wakikagua mradi wa ujenzi wa jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD) Kituo cha Afya Mateves kata ya Mateves, mradi utakaogharimu kiasi cha shilingi milioni 197.6, mpaka kukamilika kwake.
Mradi huo unategemea kutekelezwa kwa awamu kupitia fedha za Mapato ya Ndani ya halmasahuri, ambapo kwa awamu ya kwanza ulipatiwa shilingi milioni 79.1 zilizotumika kuanza jengo mpaka hatua ya gebo kwa shilingi milioni 74.9.
Akiwasilisha taarifa ya ujenzi wa Jengo hilo, Afisa Mtendaji wa Kata ya Mateves Muyai Kivuyo ameweka wazi kuwa wamepokea kiasi cha shilingi milioni 30 ikiwa ni awamu ya pili ya utekelezaji, utakaohususha shughuli za upauaji wa jengo hilo.
"Katika utekelezaji wa mradi huu wananchi wamekuwa wakichangia maji wakati wote wa ujenzi na baadaye wameahidi kitachangia gharama za kuunganisha maji kwenye jengo kutoka Mamalaka ya maji"Amefafanua Mtendaji huyo.
Aidha wajumbe hao wa Kamati wameridhishwa na utekelezaji wa mradi huo,na kuwataka viongozi wa kata hiyo, kutafuta wadau watakaowezesha kuongeza nguvu katika ujenzi huo, pamoja na kupanda miti katika kituo hicho ili kutunza mazingira.
Diwani wa Viti Maalum Mhe. Grace Seneu ameupongeza uongozi wa kata na wananchi wa kata hiyo kupitia kamati za ujenzi, kwa kusimamia vizuri mradi huo unaonesha thamani ya pesa 'value for money', kwa kuangalia hata kwa macho.
Naye Diwani mwenyeji wa kata ya Mateves Mhe. Fredy Lukumay licha ya kuwashukuru wajumbe kwa kutembelea mradi huo, amebainisha kuwa ujenzi wa Kituo hicho cha afya unategemea kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa kata ya Mateves na majirani zake.
"Ujenzi huu unakwenda vizuri, kwa kuwatumia wanakamati ambao ni wastaafu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, kusimamia ujenzi na wanafanya kwa uadilifu mkubwa kulingana na kiapo walichoapa kulitumikia taifa lao".Amesisitiza Mheshimiwa Diwani.
Ujenzi wa huo wa Kituo kipya cha Afya, ni utekelezaji wa malengo ya Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan wa kusogeza huduma za afya karibu na wanachi kwa kuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha Afya chenye hadhi.
ARUSHA DC
KaziIendelee✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.