Na Elinipa Lupembe.
Wakulima na wafugaji wadogo Kanda ya Kasazini, wametakiwa kubadili mitazamo na kuachana na kilimo cha mazoea badala yake, kuanza kutumia teknolojia mbalimbali za kilimo na ufugaji, zinazoelekezwa na watalamu, kwenye maonesho ya wakulima Nane Nane, ili kufanya kilimo cha kisasa, chenye kuzalisha mazao yenye tija kwa mkulima na taifa pia.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Omari Mgumba, wakati akifungua shughuli za Maonesho ya Nane Nane Kanda ya Kaskazini, yanayoendelea kwenye Viwanja vya Themi eneo la Njiro, Jijini Arusha kuelekea maadhimisho ya sikukuu ya Wakulima NANENANE mwaka 2020.
Naibu Waziri huyo wa Kilimo, amewasisitiza wakulima na wafugaji kufanya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia za kisasa, zinazomuwezesha mkulima mdogo kulima kisasa na kuzalisha mazao mengi na bora, kwa matumizi ya chakula na biashara kwa kujiongezea pato la familia, na kukuza uchumi wa wakulima na taifa.
"Nimejionea teknolojia nyingi za kisasa kwenye Mabanda ya maonesho, teknolojia rahisi zenye uwezo wa kumfanya mkulima, kulima kisasa na kuzalisha mazao mengi yenye ubora, niwasihi watalamu wawezesheni wakulima na wafugaji wadogo kutumia teknolojia hizo na si kuishia kwenye viwanja hivi vya maonesho" amesisitiza Naibu Waziri Mgumba.
Hata hivyo Naibu Waziri huyo, ameweka wazi kuwa, tayari serikali imekamilisha uaandaji wa maghala na vihenge vya kuhifadhia mazao ya chakula kanda ya Kaskazini, maghala ambayo yatasaidia uhifadhi wa mazao ya wakulima, pindi watakapovuna, na kusubiri mpaka bei ya mazao itakapokuwa rafiki sambamba na kuhifadhi kwa ajili ya kuongezea thamani mazao hayo kwa matumizi ya viwanda vyetu nchini, lengo likiwa kumfanya mkulima kuacha kuuza mazao yake kwa bei ya kutupa kipindi cha mavuno.
Aidha ameelezea matarajio ya serikali ya kufufua zao la ngano na shairi Kanda ya Kaskazini kwa kurejesha mashamba makubwa ya Basutu mkoani Manyara mikononi mwa serikali, mashamba amabayo yatagawiwa kwa wakulima wazawa na wawekezaji wazawa, ili watanzania waweze kutumia mashamba hayo kujiongezea kipato kwa faida yao na maendeleo ya nchi yao.
Naye mkuu wa mkoa wa Arusha Idd Kimanta amewasisitiza watalamu na taasisi zinazoshghulika na pembejeo za kilimo, kuwafuata wakulima shambani, na kuwafundisha matumizi ya teknolojia hizo pamoja na kuweka mipango rahisi kwa wakulima kumiliki teknolojia hizo na kuzitumia ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo na kumkomboa mkulima mdogo wa kitanzania.
"Kanda hii ya Kaskazini ina maeneo mengi ya kilimo yenye kuzalisha mazao ya nafaka na mbogamboga, wakulima wakiwezeshwa kutumia teknolojia za kisasa, wataondokana na kilimo kisicho na tija na kufanya kilimo biashara kwa maendeleo ya viwanda vyetu nchini" amesema Mkuu huyo wa Mkoa.
Hata hivyo, licha ya changamoto zinazowakabili wakulima, baadhi ya wakulima wameendelea kuishukuru serikali kwa kutambua mchango wao katika maendeleo ya taifa, pamoja na juhudi kubwa za kuwaunganisha wakulima na makampuni zinazozalisha teknolojia za kilimo na taasisis za fedha, jambo ambalo linazidi kuwainua wakulima na kujikita kwenye kilimo cha kisasa, kilimo kinachowakomboa wakulima wengi kiuchumi kwa sasa, tofauti na miaka ya nyuma.
Hild chondo, mkulima wa kijiji cha Kiseriani kata ya Mlangarini mkoani Arusha, amesema kuwa licha ya kuishukuru serikali kwa kuwaunganisha wakulima wadogo na taasisi zinazotoa huduma za pembejeo na watalamu wakilimo, bado wakulima wanakabiliwa na changamoto ya masoko ya mazao yao pindi wanapovuna kwa kuwa, mara nyingi bei inakuwa chini, kiasi cha wakulima wengi kuuza mazao yao kwa bei ya hasara.
Maonesho ya Wakulima kuelekea maadhimisho ya Sikukuu za wakulima mwaka 2020, yanaendeleo kwenye Viwanja vya Themi eneo la Njiro, Jijini Arusha, yenye kauli mbiu isemayo: Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora.
PICHA ZA MATUKIO KWENYE MAONESHO YA WAKULIMA NANENANE 2020 KANDA YA KASKAZINI.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.