Wakuu wa Nchi za EAC, SADC Wakutana Dar Kuleta Suluhu DRC.
Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) wamekutana Jijini Dar es Salaam Nchini Tanzania, kutafuta suluhu ya mzozo Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) uliodumu kwa zaidi ya miongo miwili mpaka sasa.
Kikao hicho kilichowakutanisha wakuu tisa wa nchi za Jumuiya za EAC na SADC pamoja na wawakilishi wa nchi wanachama wa kanda hizo, kimeketi nchini Tanzania ambapo mwenyeji wa kikao hicho ni Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika SADC.
Akizungumza wakati akifungua mkutano huo, Dkt. Samia amesema nchi za EAC na SADC hazipaswi kukaa kimya kwani zina wajibu wa kushughulikia mgogoro huo unagharimu watu wasio na hatia.
"Sote tunafahamu, DRC bado inakabiliwa na mgogoro, kama viongozi tutakaa kimya jambo hili sio zuri, nchi zetu zina wajibu wa kuhakikisha tunashughulikia changamoto hii ambayo inaathiri watu wasio na hatia, ni muhimu kutafuta suluhisho la kudumu, kama mtetezi wa amani, nchi yangu itaendelea kusaidia masuala ya kidiplomasia ili kumaliza mgogoro huu" amesema Rais Samia.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Watu wa Kenya, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mhe. William Ruto amesema mgogoro wa DRC haupaswi kushughulikiwa kwa mtutu wa bunduki bali kwa njia za mazungumzo kwa kusikilizana na kushauriana.
"Mgogoro huu hautaweza kusuluhishwa kwa njia za kijeshi, lazima tukatae kupiga mabomu, ni suluhu za kidiplomasia ndizo zinazohitajika, njia kama hiyo inahitaji kushirikisha wadau mbalimbali, mtakubaliana nami kuwa mazungumzo ya amani sio udhaifu bali ni kusikilizana na kushauriana" amesema Rais Ruto.
Rais Ruto amesema hatua za haraka zinahitajika kunusuru watu wa DRC.
"Tunaona gharama kubwa inayoikabili DRC, mamilioni ya watu wanahama, matishio ya vifo, watoto wanahusishwa katika vikosi vya majeshi, tunahitaji kuchukua hatua kwani usalama wa nchi hiyo unaathiri Dunia nzima na athari zake zinatakiwa zisipuuzwe" amesema Rais Ruto.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.