Na Elinipa Lupembe
Wananchi wa halmashauri ya Arusha, wamethibitisha utayari wao wa kuhesabiwa katika zoezi muhimu la kitaifa la Sensa ya watu na makazi, linalotegemewa kufanyika 23.08.2022.
Wananchi hao kwa makundi tofauti, wamedhihirisha utayari wao wakati wa matembezi ya hiari ya kuhamasisha zoezi hilo la Sensa ya watu na makazi, yaliyoandaliwa na halmashauri hiyo, matembezi yaliyoongozwa na Katibu Tawala wilaya ya Arumeru, Mwl. James Mchembe.
Wamesema kuwa kutokana na serikali kupitia mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan, kuhamasisha na kuelezea umuhimu wa umuhimu wa Sensa ya watu na makazi kupitia majukwaa mbalimbali, wananchi hao wamedhihirisha wazi kusubiri kwa hamu siku hiyo muhimu kwa watanzania na Taifa lao.
Athmana Idd (23) akiwakilisha vijana wa bodaboda eneo la kwa Idd, amesema kuwa serikali imejitahidi kuelezea umuhimu wa Sensa na wao kama vijana wako tayari kuhesabiwa huku wakiendelea kuhamasisha vijana wenzao na wananchi wote kuhesabiwa siku hiyo.
Nao wazee wa Ngaramtoni wamebainisha kuwa wako tayari kuhesabiwa na kuweka wazi kuwa hii sio sensa yao ya kwanza, wamekuwa wakihesabiwa kwa miaka mingi sasa hivyo wazee wengi wanaelewa sana umuhimu wa Sensa.
Mzee Lomayani Mollel (78) mkazi wa Lengijave, amesema kuwa katika maisha yake amepata kuhesabiwa mara kadhaa na kuongeza kuwa zoezi la Sensa sio geni kwake, yeye na wazee wa umri wake, wengi wanafahamu umuhimu wa Sensa na wako tayari kuhesabiwa.
Naye mwakilishi wa waumini wa wakristo, Mchungaji Charles Kingu, amesema kuwa, maandiko yatuambia Sensa ilikuwepo tangu enzi za Kaisari Agusto, wakati Bwana Yesu anazaliwa, Bikira Maria na Yusufu walikwenda Bethlehem kuhesabiwa, hivyo wakristo wanafahamu umuhimu wa sensa na wako tayari kuhesabiwa.
"Tunaona wakati huo, watu walikwenda eneo moja kuhesabiwa, lakini serikali yetu imeandaa utaratibu wa makarani kutufuata katika kaya zetu, niwatake watanzania kuona zoezi hili rahisi sana kwetu, tunafuatwa nyumbani, basi sote tuwe tayari kuhesabiwa ili kufikia malengo ya Serikali" Amesisitiza mchungaji huyo
Muumini wa dini ya kiislam Shekhe Nuru Mkwazu, amesema kuwa hata dini ya kiislam, inaelezea umuhimu wa watu kuhesabiwa, hivyo kupitia maandiko ya Kuran Tukufu waumini wa dini ya kiislamu, wanelewa maana na umuhimu wa Sensa hivyo wako tayari kuhesabiwa.
Diwani wa kata ya Olturumet Mhe. Joseph Tinayo, naye amethibitisha kuwa, wananchi wa kata yake, wametambua na kuelewa umuhimu wa Sensa ya watu na makazi na wako tayari kuhesabiwa.
Awali Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha, mhe. Ojung'u Salekwa, amefafanuwa kuwa, wananchi wa halmashauri yake, wako tayari kuhesabiwa kutokana na umuhimu wa Sensa yenye lengo la kuweka Mipango ya maendeleo kulingana na idadi ya watu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa wilaya Arumeru, Katibu Tawala wilaya hiyo, Mwl. James Mchembe, ameweka wazi kuwa Sensa ya watu na makqzi ni suala la kitaifa lenye lengo la kupanga mipango ya maendeleo kulingana na idadi ya watu, ikiwa ni nguzo kuu ya kuoamabana na maadui ujinga, umasikini na maradhi kupitia takwimu sahihi zitakapatikana kupitia zoezi hilo la Sensa.
Halmashauri ya Arusha kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ndani ya halmashauri hiyo, imefanya matembezi ya hiari kuanzia eneo la kwaIdd mpaka Standi ya mabasi Ngaramtoni lengo likiwa ni kuwahamasisha wananchi kushiriki zoezi la Sensa ya Watu na makazi 23.08.2022.
HAKIKISHA UMEHESABIWA
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.