Na Elinipa Lupembe
Mwenyekiti halmashauri ya Arusha Mhe. Ojung'u Salekwa, amewataka wananchi wa halmshauri hiyo, kuhakikisha wanatunza miti inayopandwa kwenye kampeni za upandaji miti, zinazofanyika kila mwaka katika halmashauri hiyo.
Mwenyekiti huyo ametoa rai hiyo, wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Imbibya kata ya Mwandet mara baada ya zoezi la uzinduzi wa Kampeni ya upandaji miti mwaka 2023, halmashauri ya Arusha.
Mhe. Ojung'u amefafanua kuwa, kila mwaka Serikali kwa kushirikiana na Wadau, wamekuwa na mazoezi ya upandaji miti lakini kumekuwa na changamoto kubwa katika utunzaji wa miti hiyo, inayosababishwa na wanachi wenyewe kuitelekeza na wakati mwingine kuachia mifugo kushambulia miti hiyo.
"Niwaombe ndugu zangu, madhara ya uharibifu mazingira mnayashuhudia, kupanda miti ni hatua moja tuu, miti inatakiwa kutunzwa ili ikue, tunapaswa kujitoa kusimamia miti hii, tumepanda miti elfu 10 kijijini hapa ikisimamiwa vizuri, itapunguza makali, kila mtu ana jukumu la kutunza miti iliyopandwa na kutunza pamoja na kuhifadhi mazingira yanayomzunguka". Amesisitiza Mwenyekiti Ojung'u
Hata hivyo Diwani wa kata ya Mwandet, Mhe. Logolie, licha ya kuishukuru serikali kwa kuwapa miti, amethibitisha kuwepo uharibifu wa mazingira katika maeneo ya kata yake lakini tayari wameshajiwekea mikakati ya kuhakikisha miti iliyopandwa inasimamiwa vizuri na kukua.
"Tumeandaa sheria ndogo za vijiji, mbuzi akila mti faini elfu 50, na kila mtu anapaswa kupanda miti kwenye eneo lake, ikiwemo nyumbani, shambani pamoja na maeneo ya Taasisi za Umma na binafsi". Amefafanua Mhe. Diwani.
Naye Abraham Mollel mkazi wa kijiji cha Imbibya amewashukuru wadau kwa kuwapa mmit mingi ambayo wameipanda kwenye maeneo mengi na kuahidi kuhamasishana kuitunza ili isishambuliwe na mifugo.
"Kutokana na madhara ya uharibifu tunayoyashuhudia sasa, Tumeweka sheria zetu za kutoza faini endapo mifugo itakula mti, lakini tumekubaliana kufungia mifugo yetu, ili kunusuru hali hii mbaya ya uharibifu wa mazingira, tunashukuru serikali kupitia wadau, wametuhamasisha na kutupa elimu ya umuhimu wa miti katika utunzaji wa mazingira"Amesema Abraham
Mratibu wa program hiyo MVIWAARUSHA , amesema kuwa, wanatarajia kupanda miti elfu 10 kwenye vijiji 10 vya halmashari ya Arusha, vijiji vilivyoathirika sana na ukame uliotokana na ukataji miti.
"Kauli mbiu ya Kitaifa ya Utunzaji Mazingira ya Kitaifa: Mti wangu, Nchi yangu, Taifa langu, KaziIendelee✍✍
ARUSHA DC ni Yetu, Tushirikiane Kuijenga"
PICHA ZA MATUKIO
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.