Mkuu wa wilaya ya Arumeru Jerry Muro, amewataka wananchi wa kijiji cha Engutukoit kata ya Oldonyowas, halmashauri ya Arusha, kuacha tabia ya kumzuia mwekezaji na mmiliki wa eneo lililopo kijijini hapo, kwa madai kuwa eneo hilo ni mali ya kijiji chao wakati sio kweli.
Mkuu huyo wa wilaya amewaonya wananchi hao, wakati wa mkutano wa kijiji hicho, ulioitishwa kwa lengo la kutoa kilio chao kwa mkuu huyo wa wilaya juu ya kuporwa ardhi yao na mwekezaji anayemiliki eneo hilo.
Hata hivyo baada ya mkuu huyo wa wilaya kusikiliza hoja za pande zote mbili, ilionekana mwekezaji huyo, ndio mwenye hati halali ya umiliki wa eneo hilo, baada ya watalamu wa ardhi kuthibitisha eneo hilo si mali ya kijiji bali ni mali halali ya mwekezaji huyo.
Ameongeza kuwa, wananchi wanapaswa kufuata sheria za nchi na kuwaonya kuwa kuvami eneo lolote ni kosa kisheria na kuwataka wananchi hao kuachana na tabia hiyo, badala yake kukaa pamoja na mwekezaji huyo kuona namna ya wananchi wanawezaje kunufaika kupitia uwekezaji wake.
"Ninataka mtambue kuwa eneo hilo ni eneo halali la mwekezaji huyo na anavielelezo halali vya umiliki wa ardhi kisheria, sasa namuagiza Mwenyekiti wenu kutafuta watalamu wa kumwezesha, kutambua maeneo ya kijiji chenu na kufahamu mipaka yake kwa kua amekiri mbele yenu hafahamu maeneo ya kijiji" amesema Muro
Amewasisitiza viongozi wa kijiji hicho kukaa na kuwaelimisha wananchi wao juu ya utii wa sheria za nchi pamoja na kukaa na mwekezaji huyo ili kupanga namna uwekezaji huo utakavyowaanufaisha wananchi wenu kupitia ardhi hiyo iliyo ndani ya kijiji choa.
Awali akisoma taarifa na vielelezo vya uhalali wa umiliki wa eneo hilo, Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili, halmashauri ya Arusha Khafti Tarimo, amesema kuwa, hati ya umiliki wa eneo hilo ilitolewa kwa mara ya kwanza mwa 1965 na ilikuwa ikimilikiwa na wananchi watano, ambao waliuza eneo hilo kwa kampuni ya JODISTA Ltd mwaka 1990 na baadaye, kampuni hiyo kumuuzia mwekezaji wa sasa na hati hiyo kuhamishwa miliki yake mwaka 2012 kwa kufuata kanuni, sheria na taratibu halali za umiliki wa ardhi.
Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida, wananchi wa kijiji cha Engutukoit wameibua mgogoro na mwekezaji huyo, kwa madai kuwa eneo hilo ni mali ya kijiji chao na kuzumzuia mwekezaji huyo kufanya shughuli yoyote ya kuendekeza eneo hilo na kufikia hatua ya kuwazuia hata watalamu wa halmashauri kufika katika eneo hilo.
Aidha serikali inawataka viongozi wote wa vijiji, kutambua mipaka ya vijiji vyao ikiwa ni pamoja na kuwatambua wamiliki halali wa maeneo yaliyo ndani ya vijiji vyao, sambamba na kufahamu mipango wa matumizi ya maeneo hayo ili kuepuka migogoro isiyo ya lazima baina ya wananchi na wamiliki wa maeneo.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.