Na. Elinipa Lupembe.
Wananchi wa kijiji cha Lesiraa kata ya Kisongo, halmashauri ya Arusha, wilaya ya Arumeru, wamemuomba Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mhe. Dkt. Godwin Mollel, kuwasaidi kufanya ukarabati wa jengo la zahanati ya kijiji hicho, jengo ambalo limekuwa chakavu,kutokana na kujengwa muda mrefu sasa.
Wananchi hao wametoa kilio chao, wakati Naibu waziri huyo, alipotembelea zahanati hiyo, wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Arusha, ya kukagua miradi ya afya, utoaji na upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.
Akizungumza mbele ya Naibu waziri, Mwenyekiti wa kijiji cha Lesiraa, Injinia Sakaya, amesema kuwa, jengo la zahanati hiyo, lilijengwa na wananchi mwaka 2010 na kwa sasa limekuwa na nyufa nyingi, kiasi cha kutishia usalama wa wauguzi na wagonjwa kwa kuhofia jengo hilo kuangua.
Amemuomba Naibu Waziri, kuangalia tatizo lao kwa jicho jingine, kutokana na umuhimu wa upatikanaji huduma ya afya kwa karibu,kutokana ukweli kuwa, zahanati hiyo inahudumia zaidi ya wananchi 2000, huku kukiwa, hakuna huduma za afya jirani, jambo ambalo huwalazimu kwenda haspital ya Jeshi Monduli au Kisongo umbali wa zaidi ya Kilomita 16 kwenda na kurudi.
Saitoti Lemilya, mkazi wa kijiji cha lesiraa, ameweka wazi kuwa, licha ya uchakavu wa jengo hilo, jengo hilo halina umeme pamoja na miundombinu mibovu ya barabara ya kufika kituoni hapo, hasa kipindi cha mvua.
"Nguzo za umeme zimewekwa tangu mwaka 2012, hakuna mwananchibaliyeunganishiwa umeme, mheshimiwa tusaidie tupate umeme ili kuboresha huduma za afya kwenye zahanati yetu" amesema Lemilya.
Naye Monica Saruni, amesisitiza kuwa, kina mama wajawazito wanateseka wakati wa kujifungua, hasa nyakati za usiku, muuguzi hutumia tochi kuwazalisha jambo ambalo, huhatarisha maisha ya mama na mtoto wakati wa kujifungua.
"Tunahitaji umeme ili kina mama waweze kujifungua kwa usalama, lakini pia utawezesga kupata huduma za maabara" amesema Monica.
Hata hivyo Naibu Waziri huyo, amewaahidi wananchi hao, kushughulika matatizo hayo na kufafanua kuwa, lengo la serikali ni kufikisha huduma za jamii hasa za afya karibu na wananchi, hivyo ni haki yao kupata huduma hizo na kuwataka wananchi wa Lesiraa, kuwa wavumilivu wakati serikali ikijipanga kutatua matatizo yao.
Aidha amewapongeza wananchi hao kwa kujenga zahanati hiyo, huku akiwapongeza wahudumu wa afya wa zahanati hiyo, licha ya uchakavu wa majengo lakini zahanati ni safi, vifaa vimepangiliwa vizuri na inaendelea kuwahudumia wananchi.
"Nimejionea hali halisi, lakini niwatie moyo wananchi, mkakati wa serikali ya awamu ya tano ni kusogeza huduma za jamii kwa wananchi hasa waishio vijijini, mwananchi apate huduma muhimu ndani ya kijiji chake, tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa, lakini kuweni wavumilivu, tatizo hili litakwenda kumalizika kwa ushirikiano wenu wananchi na serikali yenu makini"amesisitiza Naibu Waziri huyo.
K
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.