Wananchi wa kijiji cha Midawe, kata ya Bangata, halmashauri ya Arusha, kupitia uongizi wa awamu hii ya tano, wamekuwa na matumaini ya kufikiwa na huduma za afya kijijini kwao, huduma ambayo haikuwahi kuwepo zaidi ya miaka hamsini na tano, tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanganyika.
Matumaini hayo yamekuja, baada ya wananchi wa kijiji hicho kuamua kutoa eneo kwa ajili ya kujenga zahanati ya umma kwa wananchi wa kijiji hicho, kupitia mradi wa TASAF awamu ya III na tayari ujenzi wa zahanati kijijini hapo umeshaanza.
Wakizungumza na mwandishi wetu, alipotembelea eneo inapojengwa zahanati hiyo, wananchi hao wamekiri wazi kuwa, ujenzi huo wa zahanati umekuja wakati muafaka kutokana na adha wanayoipata ya kulazimika kutembea Kilomita tatu, kwenda kutibiwa kwenye kijiji cha jirani, hospitali ya West Meru na hospitali ya wilaya iliyo umbali wa kati ya kilomita kumi na kumi na mbili.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi ya Zahanati hiyo Loirai Ndossi, amethibitidha kuwa, kijiji hicho hakijawahi kuwa na zahanati tangu kupatikana kwa uhuru, na kuongeza kuwa uwepo wa zahanati hiyo, licha ya kuwapunguzia gharama za kutafuta huduma za afya lakini pia itapunguza vifo vya kina mama na watoto ambavyo, hutokea kutokana na kuchelewa kupata huduma.
Ameongeza kuwa kutokana na adha kubwa wanayoipata, baadhi ya wananchi wa Midawe, wakaamua kutoa eneo hili kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati hii na eneo jingine kwa ajili ya kujenga nyumba ya mtumishi wa afya.
Ester Elisha anasema kuwa, ukosefu wa zahanati kijijini kwao unasababisha kusuasua kwa baadhi ya kina mama wajawazito kushindwa kuhudhuria kliniki kwa utaratibu kutokana na umbali, jambo linalosababishwa wengine kulazimika kujifungulia nyumba au kwa wakunga wa jadi, na kuhatarisha maisha na afya ya mama na mtoto.
"Hapa kijijini baadhi wajawazito wanashindwa kuhudhuria kliniki kwa utaratibu unaofaa, kutokana na umbali na wengine kuamua kujifungulia nyumbani, mama anapata uchungu, hana hela ya kwenda hospitali Patandi au Mount Meru, analazimika kujifungua nyumbani" amesema Ester.
Alex Ngira mkazi wa Midawe ameelezea kuwa wakati mwingine, wananchi hushindwa kumudu gharama za usafiri na matibabu na kulazika kununua dawa dukani bila hata ya kupima.
"Ukingalia hela uliyonayo ni ya dawa tuu, huna nauli unaona bora nikanunue dawa nimeze, Mungu akijalia ukipona basi lakini wengine hujikuta wanapata madhara makubwa kwa kunywa dawa bila kupima" amesema Ngira.
Ndeelo Nyari amefafanua zaidi kuwa, ujenzi wa zahanati hiyo ya Midawe ni neema kwa wananchi kijijini hapo kwani wamechoka kutmbea umbali mrefu kutafuta huduma za afya na wakati mwingini watu hupoteza maisha.
"Hapa kijijini kama unavyoona ni mbali, mtu akiugua tunambeba na machela mpaka barabarani, tumepoteza wapendwa wetu sana kutokana na kijiji hiki kukosa zahanati". Amesema Nyari
Mratibu wa TASAF halmashauri ya Arusha, Grace Makema amesema kuwa, mradi huo wa zahanati umetengewa shilingi miloni 70.1 na unategemea kukamilika mwishoni mwa mwaka huu 2018.
Makema ameongeza kuwa, miradi hii inayotekelezwa na TASAF awamu ya tatu, huibuliwa na wananchi wenyewe kulingana na uhitaji na vipaumbele vyao wenyewe katika maeneo yao.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.