Na. Elinipa Lupembe.
Wananchi wa kijiji cha Laroi, halmashauri ya Arusha, wameondokana na kero kubwa ya ukosefu wa kivuko, iliyokuwa ikiwatesa kwa kipindi chote cha maisha yao, kero iliyomalizika baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja, mradi uliotekelezwa na serikali kupitia miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii - TASAF awamu ya III, kupitia miradi yake ya OPEC III.
Wananchi hao, wemethibitisha hayo wakati wa hafla fupi ya kukabidhiwa mradi huo na serikali ya mkoa wa Arusha kwa kushirikia na halmashauri ya Arusha, baada ya kukamilika, hafla iliyofanyika kijijini hapo na kusababisha nderemo na vifijo vya wanawake wa kijiji hicho, muda wote wakati wa makabidhiano.
Wamesema kuwa, kukamilika kwa mradi huo wa ujenzi wa daraja, umeleta faraja na matumaini makubwa kwa wananchi wa kijiji cha Laroi, hasa wanawake wajawazito na watoto, walioteseka kuvuka korongo hilo, wakati wa msimu wa mvua, korongo hilo likiwa limejaa maji na wakati mwingine kusababisha vifo vya wapendwa wao, watu kushindwa kitoka au kurudi nyumbani na watoto kushindwa kwenda shule au kurudi nyumbani baaa ya masomo.
Ester Lobulu, mkazi wa Laroi, amesema kuwa licha ya daraja hilo kurahisisha mawasilino ya kijiji hicho lakini pia litaokoa maisha ya watu kwa kuwa, kwa kipindi cha mvua, ndugu zao walikuwa wakipoteza maisha kwa kusombwa na maji, jambo ambalo liliwatia simanzi kubwa sana kila unapofika msimu wa mvua
"Tunaishukuru serikali na TASAF kwa kutusaidia daraja, tulikuwa tumekata tamaa, na wakati mwingine tunaichukia mvua, kwani kipindi cha mvua mawasiliano yalikatika ndani ya kijiji, na ndugu zetu walikufa, kwa sasa tunanamini watu wa Laroi hawatakufa tena" amesema Ester.
Hata hivyo, wananchi hao wa Laroi, licha ya kuishukuru serikali ya awamu ya tano, wamemuomba Rais Magufuli kuwasaidia ujenzi wa kituo cha afya, kwani kina mama wajawazito huteseka kwa kufuata huduma za afya umbali wa zaidi ya Kilomita 20 na kusababisha matatizo kwa wajawazito na watoto.
"Tunashukuru kwa daraja, kwa sasa tunapita kwa raha, watoto wetu wanakwenda shule kwa amani, lakini Baba yetu Magufuli, tunaomba usikie kilio chetu, kina mama wanajifungulia njia, huku Laroi hatuna hospitali, tunamuomba atusaidie kama alivyotusaidia daraja" amesisitiza mama Vicktoria Olais.
Awali kabla ya kukabidhi mradi huo, mgeni rasmi na Mratibu wa TASAF mkoa wa Arusha Seif Mathias, amewataka wananchi hao, kulitunza daraja hilo na kuhakikisha kila mmoja anakuwa mlinzi wa mwenzake pamoja na kuzuia kupita magari yenye uzito uliozidi uwezo wa daraja hilo, uzito wa tani 10 na si vinginevyo.
"Daraja hili ni lenu, serikali imemaliza jukumu lake, kazi yenu kubwa ni kulitumia na kulitunza, mhandisi amesema daraja linaruhusu kupita gari yenye tani 10, msiruhusu magari yenye mzigo wa zaidi ya tani hizo, ili daraja hilo lidumu na litumike kwa vizazi na vizazi, laiki pia hakikisheni mnatunza mazingira kwa kuanza kupanda miti na mikonge kuzuia mmomonyoko" amesema Mathias .
Ujenzi wa daraja hilo, umekamilika kwa ushirikiano wa Serikali na wananchi kwa gharama ya shilingi milioni 88.8, ikiwa TASAF ilitoa shilingi milioni 73, Halmashauri shilingi milioni 6.4 na wananchi wa Laroi walichangia nguvu kazi iliyothaminishwa kwa shilingi milioni 9.3.
PICHA ZA MATUKIO
Mratibu wa TASAF mkoa wa Arusha Mathias akukata utepe kufungua Daraja la Laroi.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.