Katika kuadhimisha Wiki ya Unyonyeshaji Maziwa ya Mama Duniani, Tarehe 01 hadi 07 Agosti 2025 Maafisa Lishe kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Arusha Leo 04 Agosti 2025 wameendelea kutoa elimu kwa wananchi wa Kijiji cha Laroi kuhusu umuhimu wa lishe bora kwa mama anayenyonyesha pamoja na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokumba unyonyeshaji wa maziwa ya mama.
Elimu hiyo imetolewa kupitia mikutano, kliniki za mama na mtoto, pamoja na vikao vya viongozi wa jamii, ambapo wananchi wameelezwa kuwa lishe bora kwa mama anayenyonyesha ni msingi wa afya njema kwa mtoto.
Maafisa hao wa lishe wameeleza kuwa changamoto kama vile imani potofu kuhusu unyonyeshaji, kazi nyingi za mama, kukosa msaada wa kifamilia, pamoja na hali duni ya lishe kwa mama, ni miongoni mwa sababu zinazokwamisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa ufanisi. Hata hivyo, jamii imetakiwa kushirikiana na kuunga mkono jitihada za akina mama kwa kutoa msaada wa kimwili, kihisia na kijamii ili kuwezesha mazingira rafiki ya unyonyeshaji.
Aidha, wananchi wa Laroi wamehamasishwa kutambua mchango mkubwa wa jamii katika kufanikisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama, hususan kwa kuhakikisha wanawake wanapata muda wa kutosha wa kupumzika, kula vyakula vyenye virutubisho, na kupatiwa huduma za afya mara kwa mara.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Thamini unyonyeshaji; Weka mazingira wezeshi kwa Mama na Mtoto”, ikiwa na lengo la kuhimiza familia, jamii, waajiri, na serikali kuweka mazingira yatakayomwezesha mama kunyonyesha kwa ufanisi bila vikwazo.
Kwa ujumla, wananchi wa Laroi wamepokea elimu hiyo kwa shukrani na kuahidi kuyafanyia kazi mafunzo waliyopewa ili kuboresha afya ya mama na mtoto katika jamii yao.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.