Na. Elinipa Lupembe
Wanawake na vijana wamehimizwa kuona umuhimu na kuhakikisa wanachangamkia fursa wanazoandaliwa na serikali kwenye sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kuwa wao ndio msingi wa maendeleo na mabadiliko katika sekta hiyo.
Rai hiyo imetolewa na
Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zubeir Maulid, wakati akifungua maonesho ya Nanenane kuelekea maadhimisho ya sherehe za Wakulima na Wafugaji Kanda ya Kaskazini, yanayoendelea kwenye viwanja vya Themi - Njiro mkoani Arusha
Amesema serikali imeona umuhimu wa wanawake na vijana katika sekta ya Kilimo hususani katika msingi imara wa mifumo ya chakula kuanzia shambani, sokoni mpaka kumfikia mlaji bila kikiwa salama kwa afya na kuwasisitiza kuchangamkia fursa hiyo.
"Licha ya changamoto zinazowakabili wakulima, sekta ya Kilimo, Uvuvi na Ufugaji imekuwa na mchango mkubwa katika taifa, hivyo maonesho ya Nanenane yatumike kuhakikisha teknolojia za Kilimo, Uvuvi na Ufugaji zinawafikia wananchi hususani katika kuongeza mnyororo wa thamani ili kuongeza zaidi fursa za upatikanaji wa chakula na kujenga uchumi wa mtu mmoja"Amebainisha Mhe. Spika
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella ameweka wazi kuwa, zaidi ya asilimia 60 ya watanzania wapo kwenye sekta ya kilimo wakijishughulisha na kilimo, ufugaji na uvuvi hivyo maonesho ya Nanenane ni chachu ya maendeleo kwa wakulima na huchochea uchumi wa wakulima na maendeleo ya Taifa kwa zujumla wake.
Mhe. Mongela amefafanua kuwa maonesho hayo yanazidi kuimarika mwaka hadi mwaka huku yakileta tija kwa wananchi na wakulima kwa kupata fursa elimu, ushauri wa matumizi ya teknolojia mbalimbali rahisi na za kisasa kurahisisha kilimo pamoja na upatikanaji wa masoko.
"Licha ya kuwaonesha teknolojia za kisasa za Kilimo na Ufugaji, maonesha ya Nanenane yanaendelea kuwa chachu ya mabadilika katika sekta hiyo pamoja na kuwaunganisha wakulima na wataalamu wa sekta hiyo na masoko ya mazao yao" Amesema Mkuu huyo wa mkoa
Akizungumza kwaniaba ya wakuu wa Mikoa ya Manyara na Kilimanjaro, Mkuu wa Mkoa wa Manyara Mhe. Queen Sendiga, amesema kuwa lengo la maonesho hayo ya Nanenane nikutoa elimu mubashara kwa njia ya kuona na kubadilishana uzoefu kwa wakulima na wafugaji wa mikao hiyo mitatu ili kupata uzoefu na kufanya kilimo cha kisasa chenye tija kwa wakulima na taifa.
Awali Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya Nanenane, Katibu Tawala Mkoa wa Arusha Missaile Musa amesema kuwa, maandalizi yalianza mwezi Aprili kwa kuandaa vitalu katika maeneno tofautitofauti na hatimaye kuanza rasmi tarehe 01.08.2023 yakihusisha wakulima, wafugaji, wavuvi, taasisi na makapuni ya kilimo pamoja na wadau wa sekta ya kilimo kutoka mikoa mitatu ya Kanda ya Kaskazini.
Maonesho ya nanenane Kanda ya Kaskazini 2023a mefunguliwa rasmi Agosti 3, yenye kauli mbiu ya "Vijana na Wanawake ni msingi imara wa mifumo ya chakula", na yanatarajiwa kufungwa mapema Agosti 8, 2023.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.