Wanawake wajasiriamali halmashauri ya Arusha wilayani Arumeru wamechangamkia fursa ya uanzishaji wa viwanda tangu serikali ya awamu ya tano kutangaza kutekeleza sera ya viwanda kuelekea uchumi wa kati. Hali hii imeonekana baada ya tafiti kuonesha kuwa karibu asilimia 60% ya Wanawake wajasiriamali wamejikita kwenye biashara ya usindikaji na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali shughuli wanazozifanya ndani ya nyumba zao ambazo kiuhalisia ni shughuli za viwanda vidogo.
Awali wanawake hao walikuwa wakifanya shughuli hizo bila kutambua kuwa uzalishaji wa bidhaa hizo ni viwanda vidogo mpaka hapo halmashauri kupitia Idara ya maendleo ya Jamii na Kitengo cha Biashara kuainisha na kuzitambua shughuli hizo kama viwanda vidogo.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake duniani yaliyofanyika kwenye viwanja vya ofisi za makao makuu halmashauri ya Arusha mgeni rasmi mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Dkt. Wilson Mahera amesema kuwa karibu asilimia 60% ya wanawake wajasiriamali wamejikita kwenye shughuli za uzalishaji wa malighafi na bidhaa za viwanda katika halmashauri hiyo.
Mkurugenzi Mahera ameongeza kuwa kuelekea uchumi wa viwanda Wanawake wamonesha kuwa suluhisho la uanzishaji wa viwanda katika halmashauri hiyo na kuahidi kuendelea kuwasimamia ili viwanda hivyo vidogo kuwa vya kati mpaka vikubwa.
"Tutahakikisha viwanda hivi vinakua na kuwa viwanda vikubwa kwa kuwawezesha kuongeza mitaji, kusajili na kupata vibali vyote pamoja na kuwaunganisha na maeneo ya masoko ndani na nje ya nchi" amesema Mkurugenzi Mahera. Wakizungumza wakati wa maonesho ya bidhaa, wanawake hao wamedhihirisha kuwa, licha ya kumiliki kwao viwanda vidogo bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mitaji ya kuendesha uzalishaji, usajili wa bidhaa zao pamoja na masoko ya kuuzia bidhaa zao kutokana na ushindani wa soko la bidhaa kutoka nje ya nchi. Joyce Mollel mwanamke anayejishughulisha na utengenezaji wa dawa za kusafishia vioo, amesema kuwa mtaji kwao ni tatizo jambo ambalo linasababisha uzalishaji kuwa wa kiwango cha chini ukilinganisha na uhitaji wa bidhaa sokoni. " Bidhaa zetu zinasoko kubwa ndani na nje ya nchi, tupepata soko nchini Kenya, mtaji wetu ni mdogo kiasi cha kushinda kukidhi uhitaji wa bidhaa sokoni" amesema Joyce Wanawake hao pia wamelalamikia kasumba ya watanzania kupenda kununua bidhaa kutoka nje ya nchi na kudharau bidhaa zinazotengenezwa nchini na watanzania wenzao na kuwataka watanzania kufuta kasumba hiyo badala yake kuwa wazalendo kwa kununua bidhaa za nyumbani ili kukuza uchumi wa nchi yao. Hata hivyo mkurugenzi Mahera amewahakikishia wanawake hao kuweka juhudi katika ukukusanyaji wa mapa ili kuendelea kutoa mikopo ya wanawake kupitia asilimia 4% za mapato hayo pamoja na kuwajengea uwezo wa kuweka na kukopa na kuwaunganisha na taasisi za fedha zinazotoa mikopo ya wajasiriamali kwa riba nafuu kwa wale wanaohitaji mitaji mikubwa.
Wanawake halmashauri ya Arusha wameungana na wanawake wote duniani kuadhimisha siku muhimu ya Wanawake duniani maadhimisho yaliyoambatana na maonesho ya bidhaa za wajasiriamali wanawake, upimaji bure wa afya ikiwemo kansa ya kizazi na kutoa vyeti kwa wadau wa maendeleo ya mwanamke ndani ya halmashauri hiyo, shuguli iliyosimamiwa na Idara ya maendeleo ya Jamii.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.