Na Elinipa Lupembe
Wanawake halmashauri ya Arusha wametakiwa kusimamia malezi na makuzi ya watoto sambamba na kuwa mabalozi wa kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya watoto huku wakiwa mstari wa mbele kutoa taarifa juu ya matukio hayo yanapotokea katika maeneo yao.
Hayo yamesemwa na wajumbe wa Kamati ya MTAKUWA kata ya Ilkiding'a wakati wakitoa mafunzo kwa wanawake wa kata hiyo juu ya hali halisi ya matukio ya ukatili, athari zake na namna ya kukabiliana nayo.
Afisa Maendeleo ya Jamii kata ya Ilkiding'a Anarose Shang'a amewataka wanawake wote kuwa mstari wa mbele kuwasimamia watoto kuanzia nyumbani, mtaani mpaka shuleni, ili kuwakinga na matukio ya ukatili dhidi yao.
Amesema kuwa wanawake wanayonafasi kubwa ya malezi kuanzia ngazi ya familia na jamii hivyo, wakisimama kwa nia moja matukio ya ukatili dhidi ya watoto na wanawake yatapungua na kama sio kwisha kabisa.
"Licha ya majukumu mengi waliyonayo wanawake lakini bado wanayo nafasi kubwa ya kuwasimamia watoto na wanawake wenzao kuzia na kupinga vite do vya ukatili dhidi yao, kina mama tusimame imara kuondoa ukatili kwenye maeneo yetu, tutumie dawati kutoa taarifa za matukio hayo" Amesisitiza Afisa huyo
Hata hivyo kina mama hao wamekiri kuwa na nafasi kubwa ya kuzuia vitendo hivyo kwa kuwalinda watoto kila mmoja kwa nafasi yake na kuhakikisha watoto wa kata hiyo wako salama licha ya kuwa na majukumu mengi waliyonayo wazazi kifamilia na kijamii.
Gloria Elisha amesema kuwa changamoto kubwa ni kina mama kuwa 'bize' na shughuli za kutafuta kipato na kusahau majukumu ya malezi na makuzi ya watoto na kusababisha watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili bila kujua mapema na kusisitiza kuwa elimu wanayoipata inawakumbusha kutenga muda wa kuwa karibu na watoto ili kufahamu ni changamoto wanazopitia ili kuwasaidia kufikia malengo.
Rebeca Zakayo amesema kuwa mafunzo hayo yamesisitiza mwanamke wa pembe tatu ambaye ni Mama mlezi anayetunza, kulinda na kujali familia, ni Mama mjasiriamali, anayejishughulisha kuongeza kipato cha familia na mama mshauri, anayekemea mabaya, anayeonya na anayehimiza maendeleo kwenye jamii yake.
"Tunashukuru sana elimu tuliyoipata imetukumbusha kutenga muda wa kukaa na kuongea na watoto, kuwakagua na kufuatilia maendeleo yao shuleni na kuhakikisha watoto wanapata mahitaji muhimu" Amesema Neserian Zakayo
Awali lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wanawake na kuwa na uelewa wa pamoja juu ya malezi na makuzi ili kupunguza vitendo vya ukatili na hatimaye kumaliza kabisa.
ARUSHA DC NI YETU, TUSHIRIKIANE KUIJENGA
PICHA ZA MATUKIO YA KIKAO
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.