Na. Elinipa Lupembe.
Wananchi wanaonufaika na mpango wa kunusuru kaya zenye uhitaji, halmashauri ya Arusha, mradi unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii -TASAF, wametakiwa kuhakikisha wanafuata masharti ya fedha za ruzuku wanazozipokea kutokana na utekelezaji wa mradi huo, ili kuendelee kupokea fedha hizo kulingana na idadi ya wana kaya walioandikishwa na kuingizwa kwenye mpango.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha, Seleman Msumi, kufuatia malalamiko kutoka kwa baadhi ya kaya kwa kupata fedha pungufu, ukilinganisha na hapo awali walipoanaza kupokea fedha hizo, wakati wa zoezi la uhawilishaji fedha za ruzuku ya mwezi Mei na Juni 2021, zoezi lililofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Mkurugenzi huyo ametoa ufafanuzi masharti yayopaswa kuzingatiwa na kaya zilizo kwenye mpango, kwa kuwasisitiza wakuu na wasimamizi wa kaya hizo, kuwa fedha hizo za ruzuku zinatolewa kwa kaya zao, zikiwa na masharti ambayo kila kaya inapaswa kuyazingatia, na kuwasisitiza wanakaya hao kuzingatia masharti hayo, ili waweze kuendelea kuwa na sifa za kunufaika na fedha hizo, na kuweza kufikia lengo lililokusudiwa na serikali la kuondokana na umasikini iliyokithiri ndani ya jamii.
Ameyataja masharti hayo ni pamoja na ruzuku ya msingi inayotolewa kwa kaya bila masharti yoyote, ruzuku ya afya inayotolewa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 5, yenye masharti ya watoto hao kupelekwa kliniki zilizo karibu na maeneo wanayoishi, huku ruzuku ya elimu ikiwahusu watoto wanaosoma shule za msingi na sekondari ikiwa na sharti la kuwa watoto hao kuhudhuria shuleni kwa kipindi chote cha masomo yao.
Ameongeza kuwa, ili kaya iendelee kuwa na sifa ya kupokea ruzuku ya elimu, kaya inapaswa kuhakikisha watoto wanahudhuria shuleni kwa muda wote, kwa majina yao sahihi yaliyoingizwa kwenye mpango na shuke walizoandikishwa, huku ruzuku ya afya ikiwataka, kuwapeleka watoto wa chini ya miaka mitano kliniki, lengo likiwa ni kuimarisha afya za watoto wa wanakaya zenye uhitaji, kushindwa kutimiza masharti hayo kunamuondolea mwanakaya sifa na serikali kuondoa ruzuku hiyo kwenye mwanakaya husika.
"Fedha hizi za ruzuku, zinakuja na masharti yake, hakikisheni mnatimiza masharti hayo, TASAF inafuatilia shule anayosoma mtoto, asipooneka kuhudhuria shuleni, ruzuku hiyo inaondolewa, sambamba na mtoto wa chini ya miaka mitano asipohudhuria kliniki, ruzuku inaondolewa pia, niwatake wana kaya kuhakikisha mnazingatia masharti hayo kwa kuhakikisha wanafunzi wanahudhuria shule na kuwapeleka kliniki watoto wa chini ya miaka mitano" amesema Mkurugenzi Msumi.
"Kushindwa kufuata masharti hayo yaliyoainishwa, kunaondoa sifa ya mwanakaya kuwepo kwenye mpango na kuondoa ruzuku ya fedha zinazotolewa, hivyo kuweni makini kwa kuzingatia masharti hayo ili kaya zenu ziendelee kunufaika na ruzuku hiyo inayotolewa na serikali" amesisitiza
Hata hivyo, mratibu wa TASAF halmashauri ya Arusha, Grace Makema, amezisisitiza kaya hizo zenye uhitaji, kutumia pesa hizo za ruzuku kuinua pato la familia zao, kwa kuanzisha miradi midogo midogo ya kilimo, mifugo na biashara ndogo ndogo, miradi ambayo itawezesha kaya hizo kujipatia mahitaji ya msingi kama chakula, mavazi na malazi na kuonsokana na lindi la umaskini uliokithiri upunaozikabili kaya hizo.
Naye Ana Mollel, mlengwa wa kaya zenye uhitaji, amekiri na kuthibitisha kuwa baadhi ya wanakaya wamekuwa wazembe kuwapeleka watoto wenye umri wa chini ya miaka kliniki kwa muda wote, huku wengine wakishindwa kuhimiza na kufuatilia mahudhurio ya watoto wao shuleni, jambo linalosababisha kukosa ruzuku za elimu na afya, na kusisitiza kuwa, watalamu wasichoke kutoa elimu kwa wanakaya hao, juu ya umuhimu wa kuzingatia masharti ya ruzuku hizo kwa kuwa baadhi ya wanakaya kuwa wazembe.
Awali halmasahuri ya Arusha imefanikiwa kuhawilisha fedha za ruzuku kiasi cha shilingi milioni 293.4, kwa jumla ya kaya 8,112 ndani ya vijiji 45 vilivyo kwenye mpango na kufikisha jumla ya shilingi bilioni 1.8 kwa mzunguko wa sita wa TASAF awamu ya pili.
ARUSHA DC
#KaziInaendelea.
PICHA ZA MATUKIO
Wanakaya wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya zenye uhitaji kijiji cha Ilkisongo wakitia saini, mara baada ya kupokea fedha za ruzuku ya mwezi Mei na Juni 2021.
Wanakaya wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya zenye uhitaji kijiji cha Ilkisongo wakisubiri kupokea fedha za ruzuku ya mwezi Mei na Juni 2021, kutoka kwa Afisa Maendeleo ya Jamii Getrude Darema ( aliyekaa) wakati wa zoezi la uhawilishaji fedha.
Wanakaya wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya zenye uhitaji kijiji cha Ilkisongo wakiwa kwenye mstari, tayari kwa kupokea fedha za ruzuku ya fedha ya mwezi Mei na Juni 2021.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.