Na Elinipa Lupembe
Wananchi walio kwenye Mpango wa Kunusu Kaya Masikini kipindi cha pili awamu ya tatu, mradi unaotekelezwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Halmashauri ya Arusha, wamekiri kuanza kuondokana na wimbi la umasikini uliokithiri, uliokuwa ukizikabili kaya zao na kuwa na mwelekeo wa kufikia malengo ya mpango huo.
Wanufaika hao wamekiri fedha hizo, kuwezesha kuondokana na wimbi la umasikini lililokuwa likizikabili kaya hizo, kwa kuanza kukuza kipato cha kaya na kuwezesha kaya kukua kiuchumi na kijamii huku watoto wakipata huduma za afya na elimu kwa amani na furaha, tofauti na hapo awali.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti wakati wakupokea ruzuku ya dirisha la 6, wanufaika wa kijiji cha Oloigueruno kata ya Ilkiding'a, wamekiri fedha hizo za ruzuku kuwezesha kukuza kipato cha kaya kwa kuanzisha miradi na biashara ndogo ndogo.
Helena Lukumai (37), anayejishughulisha na bishara ya uuzaji wa viatu, amesema kuwa, pesa ya TASAF ndio imemuwezesha kupata mtaji wa kuuza viatu na tangu alipoanza kupokea pesa hizo alizikusanya mpaka kufikia shilingi elfu 80 na kupata mtaji wa kuanzisha biashara ya kuuza viatu.
Ameweka wazi kuwa awali hali ya maisha ya kaya yake haikuwa nzuri, hata kupata chakula cha familia ilikuwa ni changamoto, lakini kwa sasa ana uhakika wa famila yake kupata milo mitatu pamoja na kujikimu na mahitaji mengine ya nyumbani.
Naye Judith Paulo amebainisha kuwa, alianzisha mradi wa genge la kuuza mbogamboga, genge ambalo linafanya vizuri na kwa sasa kaya yake ina uhakika wa maisha, watoto wanapata chakula na mahitaji mengine kupitia genge hilo.
Neema Saitabau kijiji cha Lemanda, anyejishughulisha na biashara ya kuuza viazi soko la Oldonyosmabu, amesema kuwa, alikusnaya pesa za alizopokea TASAF na kupata elfu sitini na kuanza biashara ya kuza viazi kwenye magulio ya Oldonyosambu na Ngaramtoni.
"Nilianza na gunia moja kwa sasa nina mtaji wa magunia matatu, ninauza kwenye masoko ya Oldonyosambu na Ngaramtoni na ninategeme mtaji ukiongezeka kwenda kwenye masoko mengine zaidi". Amesisitiza Neema
Hata hivyo wanufaika hao wameishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na mama Samia Suluhu, kwa kutoa elimu bila malipo mpaka kidato cha sita, jambo ambalo wamekiri kusaidia watoto wa kaya za walengwa wa TASAF, kuwa na uhakika wa masomo mpaka kidato cha sita kama ilivyo kwa watoto wengine.
"Zamani ilitulaizimu kutumia pesa hii ya TASAF kulipia watoto ada na michango mingine shuleni, baada ya serikali kuviondoa vyote, tumepata ahueni sana, pesa hizi zinatumika kufanya shughuli nyingine za kutuingizia kipato, kiukweli serikali imeturahisishia maisha kwa kiasi kikubwa mno".Amefafanua Anna Pendaeli
Naye Mratibu wa TASAF halmashauri ya Arusha, Grace Makema, amesema kuwa, kwa mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya shilingi bilioni 2. 8 zimetumika kulipa walengwa hao kwa madirisha 6 huku jumla ya kaya 13,920 kutoka vijiji vyote 88 vya halmashauri hiyo zikinufaika na kuongeza kuwa, malipo yanayofanyika sasa ni dirisha la 6 na jumla ya shilingi milioni 568.8 zimegawiwa kwa kaya hizo.
Ikumbukwe kuwa lengo la Mpango wa kunusuru kaya Masikini kipindi cha pili cha awamu ya tatu mwaka 2020 mpaka 2023 ni kutoa fursa za kuongeza fursa za kujiongezea kipato na kuboresha huduma za kiuchumi na kijamii kwa kaya za walengwa pamoja na kulinda maslahi ya watoto kiafya na kielimu.
*SHIRIKI SENSA YA WATU NA MAKAZI*
*JIANDAE KUHESABIWA 23 AUGUSTI 2022*.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.