Kamishna wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mheshimiwa Dkt. Zakia Mohamed Abubakar, amefanya ziara ya kutembelea mafunzo ya Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, Jimbo la Arumeru Magharibi. Leo Tarehe 06 Agosti 2025
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Dkt. Zakia aliwapongeza Wasimamizi Wasaidizi kwa kushiriki kikamilifu kwenye mafunzo hayo, ambayo yalianza rasmi tarehe 04 Agosti 2025. Alieleza kuwa ushiriki wao ni hatua muhimu katika kuhakikisha maandalizi ya uchaguzi wa mwaka 2025 yanafanyika kwa ufanisi na kwa kuzingatia misingi ya haki na uwazi.
Aidha, Dkt. Zakia alisisitiza umuhimu wa Wasimamizi Wasaidizi kuzingatia kikamilifu kanuni, taratibu na maadili ya uchaguzi, kama wanavyofundishwa katika mafunzo hayo. Alieleza kuwa utekelezaji wa majukumu yao unapaswa kuendeshwa kwa uadilifu, weledi, na kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyowekwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
"Ni muhimu sana kwa kila mmoja wenu kuhakikisha kuwa mnatumia vizuri mafunzo haya kwa kuyatekeleza kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa. Huu ni uchaguzi chini ya Tume Huru ya Uchaguzi, hivyo tunategemea ubora na uwajibikaji wa hali ya juu kutoka kwenu," alisisitiza Dkt. Zakia.
Mafunzo haya ni sehemu ya maandalizi ya awali ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, na yanalenga kuwajengea uwezo Wasimamizi Wasaidizi katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika ngazi ya kata.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.