Kufuatia Kauli mbiu ya siku ya mtoto wa Afrika mwaka 2018, inayosema 'KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA:TUSIWAACHE WATOTO NYUMA', watoto wameiomba serikali kutatua changamoto nyingi zinazowakabili ambazo zinakwamisha maendeleo na ustawi wa watoto, kuelekea uchumi wa viwanda.
Rai hiyo ya watoto, imetolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Tanzania, Joel Festo wakati akiwasilisha maazimio ya watoto, kwenye Kongamano la watoto mkoa wa Arusha, lililofanyika kwenye ukumbi wa Lake Nyasa ndani ya kituo cha kimataifa cha mikutano AICC.
Mwenyekiti Joel amesema kuwa, changamoto zinazowakabili watoto kwa sasa, zinatakiwa kudhibitiwa na kutafutiwa ufumbuzi, endapo hazitatafutiwa ufumbuzi endelevu, zinaweza kuleta madhara makubwa kwa maisha ya watoto baadae na watoto kushindwa kufikia malengo ya kutekeleza uchumi wa viwanda.
Mwenyekiti huyo amezitaja baadhi ya changamoto hizo ambazo ndio maazimio ya Baraza la watoto kuwa, ni pamoja ukosefu wa miundombinu ya shule isiyorafiki, ambayo inakwamisha tendo la kujifunza na kusababisha watoto wengi, kushindwa kufanya vizuri katika masomo, huku hali hiyo ikitishia watoto hao kutokuendana na matarajio ya serikali ya kuwa na wasomi wa kimkakati, kuelekea kwenye uchumi wa viwanda.
Joel ameendelea kueleza kuwa, vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinavyofanywa na jamii, ajira za watoto hasa watoto wanaoishi maeneo ya migodini na kwenye mashamba makubwa, kukeketwa, mimba na ndoa za utotoni, haviwezi kuwafanya watoto kufikia uchumi wa viwanda unaoandaliwa na serikali kwa sasa.
Ameongeza kuwa, watoto bado wanachangamoto ya ushirikishwaji hafifu wa kutoa maamuzi kuanzia ngazi ya familia, Huduma za afya kwa watoto hasa maeneo ya vjjini, adhabu kali zenye madhara kwa watoto,pamoja na mahakama zisizo rafiki za kuuendeshea mashauri na kesi za watoto.
" Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya, baba yetu, watoto wanakuomba, kutatua changamoto hizo ili kuwaandaa watoto hawa, kuelekea kwenye uchumi wa viwanda, kwani watoto wa Tanzania, wanayo matarajio makubwa ya kutekeleza uchumi huo pindi watakapokuwa watu wazima" amesema Mwenyekiti Joel.
Hata hivyo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, mheshimiwa Faustine Ndugulile amesema kuwa serikali inafahamu changamoto za watoto na imeweka mikakati thabiti ya kutatua changamoto hizo kisekta.
Mpaka sasa serikali pamoja na kutoa elimu bila malipo lakini pia, inaendelea kuboresha miundombinu ya shule na kuwa na mazingira rafiki ya kujifunzia ili kupata wasomi wa kuendeleza taifa hili.
Ameongeza kuwa serikali, imeandaa sera na sheria ya mtoto huku ikianzisha mahakama za watoto zenye mazingira wezeshi ya kufanyia mashauri ya watoto, mahakama zitakazoshughulikia mashauri ya matukio ya ukatili dhidi ya watoto,pamoja na kuwa na jela maalum ya watoto ambayo watoto wataendelea kupata haki zote za msingi wakiwa huko.
"Serikali inatambua changamoto za kufanya mashauri ya watoto kwenye mahakama zilizopo, kwa sasa kutakuwa na mahakama za watoto zenye mazingira huru kwa mtoto, zaidi kutakuwa na jela za watoto". Amesema Naibu Waziri
Naibu Waziri huyo, amefafanua kuwa licha ya serikali kuweka mikakati hiyo, ameitaka jamii kushirikiana na serikali, kuwaandaa watoto kuelekea uchumi wa viwanda kuanzia ngazi ya familia, kwa kuwapa haki zote za msingi huku jamii ikiwa na kazi kubwa ya kuwalinda watoto.
Aidha amewataka watoto wenyewe kujilinda na kutambua haki zao na kutoa taarifa pale wanapofanyiwa vitendo vya ukatili kupitia namba maalumu ya 116 na kupitia kwa viongozi wa maeneo wanayoishi na kutumia madawati ya malakamiko yaliyoanzishwa shule.
"Watoto serikali yenu inawapenda na kuwajali, msiogope na wala msikubali kunyamazishwa na mtu yoyote pale unapofanyiwa aina yoyote, serikali ipo kwa ajili yako na itakulinda" amesisitiza Naibu Waziri
Awali katika kongamano hilo, watoto wamepata fursa ya kujadili mambo mbalimbali yanayowahusu huku wakijengewa uwezo wa namna ya kukabiliana na changamoto zinazowakabili hasa ukatili dhidi yao.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.