Na.Elinipa Lupembe.
Wazazi halmashauri ya Arusha, wametakiwa kufahamu kuwa, wana wajibu mkubwa wa kulinda watoto wao, dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyoweza kufanyika ndani ya familia na jamii zao, licha ya kwamba serikali imeweka mipango mikakati mingi ya kupambana na ukatili dhidi ya watoto na wanawake.
Rai hiyo imetolewa na mkurugenzi mtendaji, halmashauri ya Arusha na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mtoto ( MTAKUWA) ngazi ya halmashauri, Selemani Msumi, wakati wa kikao kazi cha kuzijengea uwezo kamati za MTAKUWA ngazi ya kata, kilichofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo, mafunzo yaliyoandaliwa na shirika la CWCD la mkoani Arusha.
Mkurugenzi huyo amesisitiza kwamba, wazazi ndio walinzi wa kwanza wa mtoto, kutokana na uhalisia kwamba matukio mengi ya ukatili yanafanyika nyumbani na watu wa karibu wa familia, hivyo ni wajibu wa wazazi kujipanga vema, kukabiliana na kudhibiti vitendo hivyo vya ukatili kwa watoto ndani ya familia ama ndani ya kaya zao.
"Tafiti zinaonyesha asilimia 75 ya vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto vinafanyika nyumbani na vinafanywa na watu wa karibu wa familia, ikiwemo baba, kaka, mjomba, wasaidizi wa kazi, pamoja na wageni wa familia, jambo ambalo wazazi tukijipanga vyema, tunaweza kudhibiti vitendo hivyo vya ukatili kuanzia nyumbani, wazazi tuone namna ya kuwakinga watoto wetu kwa kuwa karibu nao, jukumu hilo lipo ndani ya uwezo wetu na si vinginevyo" amesisitiza Mkurugenzi Msumi.
Naye Mkurugenzi wa shirika la CWCD, mama Hindu Mbwego, amesema kuwa, kupitia kamati za MTAKUWA ngazi za kata na vijiji, jamii imeanza kufahamu umuhimu wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto, licha ya changamoto zilizopo lakini jamii imeanza kuripoti matukio ya ukatili kwenye vyombo husika vya kisheria na baadhi ya watoto wameweza kupata haki zao kupitia mahakama.
Hata hivyo, Mama Hindu amesema kuwa, licha ya kuwa shirika limefanikiwa kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati za MTAKUWA ngazi ya wilaya na kata, lakini wameanza kuangalia namna ya kuziwezesha kamati hizo kutumia rasilimali zilizopo ndani ya kata zao, katika harakati za kupambana na matukio ya ukatili, badala ya kutegemea mashirika na serikali peke yake.
"Kamati za MTAKUWA zinatakiwa kujipanga kuanza kuatfuta rasilimali zao ndani ya kata, kupitia wananchi wa eneo husika, watu mashughuli, viongozi wa chama na serikali, wadau wa maendeleo ndani ya kata, badala ya kitegemea mashirika na serikali peke yake, kila mtu ndani ya kata akifahamu kuwa, ana jukumu la kupambana na ukatili dhidi ya wanawake na watoto, atawajibikwa kwa hali na mali, iwe kama kwenye misiba, ambapo kila mwanajamii analazimika kushiriki" amesisitiza mama Hindu.
Afisa Maendelo ya Jamii, halmashauri ya Arusha, Angela Mvaa, ameweka wazi kuwa, kamati za MTAKUWA katika halmashauri hiyo, zimeanza kuleta matokea chanya, kwa jamii kufahamu ukatili ni nini, madhara ya ukatili, namna ya kutoa taarifa pindi mtoto anapofanyiwa ukatili kwa mamalaka husika lakini zaidi ndoa za utotoni zimepungua kwa kuwa watoto wa kike wameendelea na masomo tofauti na hapo awali, mabinti wengi walikatizwa masomo kwa kupata mimba ama kuozwa, kutokana na mila na desturi.
Naye Afisa Mtendaji kata ya Mwandeti, Aron, amesema kuwa licha ya juhudi za serikali na wadau wa maendeleo kuzijengea uwezo kamati za MTAKUWA ngazi ya kata, bado kuna uhitaji wa kuzijengea uwezo kamati za MTAKUWA ngazi ya vijiji ili kwa pamoja wakiungana kazi itakuwa rahisi zaidi na hata kuifikia jamii kwa ukubwa wake.
Aidha Mtendaji Aroni, ameipongeza serikali kwa kuwa na sera zenye mikakati thabiti ya kupambana na ukatili dhidhi ya wanawake na watoto, mikakati ambayo kwa kushirikiana na wadau wa ASAS za kiraia, sasa imeanza kuzaa matunda, hasa katika jamii za kimaasai ambazo zilikuwa kama zipo gizani, kutokana na mila na desturi za kabila hilo.
Awali shirika la CWCD kwa kushirikiana na halmashauri ya Arusha, wamefanya mafunzo ya kuzijengea uwezo kamati za MTAKUWA kwa kata 7 za Kinyaki, Lengijave, Mwandeti, Oloirieni, Ilkiding'a, Olturoto na Bangata, lengo likiwa kuziwezesha kamati hizo kutumia rasilimali ndani ya kata zao kwa kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
ARUSHA DC
#kaziinaendelea ✍✍
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.