Na Elinipa Lupembe.
Wazazi wenye watoto shule ya sekondari Oldonyowas, halmashauri ya Arusha, wametakiwa kukaa na kutafakari namna bora, ya kuwapatia watoto wao chakula cha mchana wawapo shuleni.
Rai hiyo imetolewa na Kaimu mkurugenzi, halmashauri ya Arusha, Anastazia Tutuba, wakati wa hafla fupi ya kukabidhiwa majengo ya shule hiyo na wadau, waliofadhili ujenzi wa majengo shuleni hapo, mara baada ya mkuu wa shule hiyo, kuwasilishwa changamoto ya ukosefu wa chakula cha mchana kwa wanafunzi.
Kaimu mkurugenzi huyo amesema, anasikitishwa sana kusikia wanafunzi, wanafika shuleni saa moja mpaka saa kumi jioni, bila ya kula kitu chochote huku wazazi wakipongezana kwa kuchanga fedha na kujenga shule.
Amesema kuwa shule hiyo ni mpya, ina mandhari nzuri na mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia, endapo watoto hao watashinda njaa, wasitegemee ufaulu kwa wanafunzi hao, badala yake nguvu zao walizowekeza kwenye ujenzi wa shule hiyo, zitakuwa zinapotea bure.
"Mtoto hawezi kufanya vizuri kwenye masomo akiwa na njaa, kwani mtu anaposoma ubongo unapoteza 'carolis' nyingi kuliko mtu anayelima, sasa ili nguvu mlizowekeza shuleni hapa ziweze kuzaa matunda bora kitaaluma, ni lazima muwape watoto hawa chakula cha mchana wawapo shuleni" amesema Kaimu mkurugenzi huyo.
Awali mkuu wa shule hiyo, mwalimu Richard Mugabiso, akisoma risala fupi ya shule hiyo mpya iliyoanza Januari mwaka huu, amethibitisha kuwa, licha ya shule hiyo kujitosheleza kwa miundombinu na walimu, changamoto kubwa ni wanafunzi kutokupata chakula cha mchana wawapo shuleni, jambo linalotokana na wazazi kutokuchangia chakula hicho.
Mkuu huyo wa shule ameonyesha hofu yake, inayoweza kuchangia watoto hao kushindwa kufanya vizuri kitaaluma, kutokana na wanafunzu hao kushinda njaa, kutwa nzima na kuwataka wazazi kuliangalia na kulitafakari suala hilo upya.
Hata hivyo sera ya elimu bila malipo, imefafanua jukumu la wazazi ni kumpatia mtoto mahitaji yake binafisi ikiwemo chakula cha mchana kwa shule za kutwa, madaftari, nauli ya kwenda na kurudi shuleni.
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Oldonyowas, Geofray Ayo amesema kuwa, wazazi wa kijiji cha Oldonyowas, wanajitoa sana kuchangia maendeleo ya shule ikiwemo chakula cha watoto wao, lakini changamoto kubwa ni wazazi wenzetu wa vijiji vya jirani, wao hawachangii chakula jambo ambalo linasababisha kukosekana kwa chakula.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo amasema, wamepanga kukutana na viongozi wa vijiji jirani ambavyo wanafunzi wanatokea, ili kupanga mkakati wa kuchangia chakula cha wanafunzi.
Kaimu mkurugenzi halmashauribya Arusha, Anastazia Tutuba akizungumza na wananchi wa kijiji cha Oldonyowas, wakati wa makabidhiano ya majengo ya shule ya sekondari Oldonyowas.
Mwenyekiti wa kijiji cha Oldonyowas, mheshimiwa Geofray Ayo, akisoma taarifa ya shule ya sekondari Oldonyowas, wakati wa makabidhiano ya majengo ya shule hiyo.
Wanafunzi wa shule ya sekondari Oldonyowas, wakiwa kwenye hafla ya makabidhiano ya majengo ya shule ya sekondari Oldonyowas.
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.