Waziri wa Nchi, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Angellah Kairuki ametangaza waombaji 18,449 wa ajira mpya waliochanguliwa na kupangiwa vituo vya kazi katika kada ya ualimu na afya huku akitoa maelekezo nane mahsusi.
Mhe. Kairuki akizungumza Juni 5, 2023 jijini Dodoma kuhusu ajira mpya 21,200 zilizotangazwa Aprili 2023, amesema kati ya waombaji hao 18,449 waliochaguliwa 5,319 ni wa kada za afya na kada za ualimu ni 13,130.
“Mtakumbuka Mtakumbuka kuwa mwezi Aprili, 2023; Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa kibali cha ajira ya watumishi 21,200 kati yao 13,130 walikuwa wa kada ya Ualimu na 8,070 wa kada za Afya.”
“Hata hivyo, mchakato wa kukamilisha uchambuzi wa maombi katika jumla ya nafasi 2,751 za kada ya afya unaendelea, na utatangazwa punde utakapokamilishwa,”amesema.
Waziri Kairuki amesema katika maombi 171,916 yaliyopokelewa waombaji 86,448 waliokidhi vigezo na 18,449 ndio walichaguliwa na kupangiwa vituo vya kazi.
Amewaagiza waajiriwa wapya kabla ya kuripoti kwenye vituo vya kazi walivyopangiwa, wanatakiwa kuripoti kwa Wakurugenzi wa Halmashauri na nyaraka halisi na atakayechukua posho ya kujikimu na baadaye asiripoti katika kituo chake cha kazi alichopangiwa atachukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ikiwa ni pamoja na kushtakiwa kwa kosa la kujipatia fedha au mali kwa njia ya udanganyifu.
“Waajiriwa wapya ambao hawataripoti katika vituo walivyopangiwa ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya tangazo hili, watakuwa wamepoteza nafasi zao na nafasi hizo zitajazwa na waombaji wengine wenye sifa waliopo kwenye kanzidata ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI,”amesema.
Pia amesema waajiriwa hao hawaruhusiwi kubadilisha kituo na kuomba uhamisho kabla ya kutimiza miaka mitatu, watatakiwa kusaini mkataba wa kufanya kazi katika vituo hivyo si chini ya miaka mitatu.
Mhe.Kairuki amewaelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri ambazo waajiriwa wapya wamepangiwa kuhakikisha wanawawezesha wa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya utumishi wa umma na baadaye kutoa taarifa ya kuripoti kwa watumishi hao.
Naye, Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka TAMISEMI, Dk. Ntuli Kapologwe amefafanua ajira za kada za afya ambazo zitatangazwa tena kutokana na kukosa waombaji wenye sifa stahiki kuwa ni za Wataalamu wasaidizi wa viungo, wataalamu wa kuendesha mitambo ya x-ray na Maofisa Tabibu wasaidizi kwa ngazi ya astashahada ambao uzalishaji wake bado ni mdogo.
SOURCE :ORT- TAMISEMI
Sekei Road
Anuani ya posta: 2330 Arusha
Simu : +255 027 2502737
Simu: 073 65000476
Barua pepe: ded@arushadc.go.tz
Copyright ©2018 Arushadc . All rights reserved.